0

Siku kadhaa zilizopita nieleza namna ambavyo utaweza kuzitambua fursa mahali ambapo unapoishi, na siku ya leo nitaeleza kitu cha kuzingatia pale uonapo fursa.

Jifunze kupitia hadithi hii;
Ilikuwa ni majira ya asubuhi, ambapo hali ya hewa haikuwa shwari, mawingu mazito yaliyoambatana na radi pamoja na ngurumo ndizo ambazo zilikuwa zimetawala siku hiyo.

Wanyama wengi walishukuru sana kwani walidhani mvua kubwa ingenyesha siku hiyo kwani ni siku nyingi zilipita bila mvua kunyesha na kupelekea baadhi ya mazao yaliyokuwako shambani kuendelea kunyauka.

Hata hivyo cha ajabu pamoja na kuwako kwa hali hiyo yenye ishara ya kunyesha mvua kubwa itanyesha, lakini mvua haikuweza kunyesha. Kila Mnyama alisikitika sana kutokea kwa hali hiyo. Kadri siku zinavyozidi kwenda njaa kali ilitawala mahala pale hata kupelekea kwa idadi kubwa ya wanyama wengi kufa.

Kati ya wanyama walioathiriwa na hali hiyo ni fisi, kwani  ndiye alikuwa mnyama mwenye watoto ambao walikuwa ni bado wadogo hivyo hawakuwa na uwezo wa kujitafutia chakula hivyo ilimpasa fisi huyo kila wakati kwenda kutafuta chakula kwa ajili ya wanae.

Fisi huyo pamoja na kuwako kwa hali ngumu ambayo iliwatala mahali pale, kila alipojaribu kuwinda alikuwa anapata kitoweo kidogo sana ambacho kutokana na idadi kubwa ya watoto ambao alikuwa akiwamiliki kitoweo hicho kilikuwa hakiwatoshi watoto wake.

Kuna wakati zilipita siku tatu mvululizo bila ya kupata kitu chochote, hata kupelekea watoto wake kudhoofu sana. Kutokea kwa hali ile kulimchanganya sana mama fisi.

Siku moja mnamo usiku wa maneno watoto wa fisi kutokana na njaa ambayo walikuwa nayo waliweza kulalamika kwa mama yao ya kwamba njaa kali inawasumbua sana hivyo ingefaa kwa mama yao aende mawindoni angepata chochote ambacho kiwafaa kwa siku ile.

Pasipo kupoteza muda mama fisi alifanya kama ambavyo wanawe walimtaka afanye japo ilikuwa ni majira ya usiku. Mama fisi aliaamka na kuanza harakati za kutafuta chakula usiku ule, japo usiku ule haukuwa na giza kubwa kwa sababu kulikuwa na mbalamwezi ambayo ilimsaidia kumpa mwanga wakati wa mawindo yake.

Mama fisi alizunguka sana usiku ule pasipo kupata chochote. Lakini kadri alivyozidi kutembea kwa mbali aliona kama maji. Baada ya dakika chache kufika mahali pale cha ajabu alikutana na kisima ambacho kilikuwa kimejaa maji.

Mama fisi alimshukuru sana Mungu kwa kuyaona maji yale kwani alikuwa amebanwa sana na kiu pamoja na njaa isiyoelezeka. Hata hivyo wakati mama fisi akitaka kunywa maji yale aliona kitu ambacho kinaelea juu ya maji.

Mama fisi alijaribu kufanya uchunguzi juu ya kile kitu ambacho kilikuwa kinaelea, kadri alivyozidi kufanya uchunguzi aligundua kwamba ulikuwa ni mfupa. Mmmh si unajua tena fisi na mfupa.

Mama fisi pasipo kupoteza muda alijitupa ndani ya maji kwa ajili ya kuuchukua mfupa ule. Lakini pamoja na kufanya uchunguzi wake wa kina ukweli ni kwamba kilichokuwa kikielea juu ya maji haukuwa mfupa bali ilikuwa ni mbalamwezi.

Baada ya kuingia kwenye kisima kile mama fisi alishangaa kuona hakuna mfupa ambao aliuona wakati yupo nje ya maji. Na kwa kuwa kisima kilikuwa ni kirefu sana mama fisi hakuweza kutoka hivyo alikufa ndani ya kisima kile.

Watoto wa mama fisi walisubiri kwa siku kadhaa bila mafanikio ya mama yao kurudi, hivyo na wao waliliwa na wanyama wengine. Na historia ya mama fisi pamoja na wanawe ikaishia pale.

Tafsiri ya hadithi hii ni nini?
Ukweli ni kwamba watu wengi hulalamika katika mambo ambayo huwa wanayaanzisha, na mwishowe wanajikuta wanashindwa katika mambo hayo. Lakini moja ya tatizo kubwa ambalo hufanya kutokea kwa hali hiyo ni;
Kutofanya uchunguzi wa fursa ambazo unazoziona, hili ndilo tatizo kubwa sana ambalo huwakumba watu wengi sana.

Unakuta mtu anaiona fursa fulani na fursa hiyo ana uhakika kwa kiwango kikubwa kuweza kibadili maisha yake kwa kiwango cha hali ya juu lakini cha ajabu unakuta mtu anashindwa sana katika fursa hiyo kwa sababu hakufanya uchunguzi wa kutosha juu ya fursa hiyo.

Huenda ukawa unataka kufanya jambo fulani la msingi sana katika maisha yako, lakini nikwambie jambo moja ya kwamba usikurupuke bali tafakari kwa kina kuhusu faida na changamoto ya jambo hilo.

Hivyo jambo la msingi ambalo ni vyema kulizingatia ili uweze kufanikiwa unahitaji kufanya uchunguzi wa kutosha kwa kila fursa ambayo unaiona. Kwani endapo hautafanya hivyo ipo siku utalalamika tu , pia utayaathiri maisha yako na watu wengine kama tulivyoona kwa fisi.

Post a Comment

 
Top