0

BAADHI ya wadau wakuu wa Tasnia ya Habari wameendelea kugomea kutoa maoni yao mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari wa mwaka 2016, baada ya ‘kukacha’ kuhudhuria kikao maalumu cha kamati hiyo cha kupokea maoni yao, huku Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kikiwasilisha maoni yake.

Kutokana na TLS kuwa wadau pekee waliowasilisha maoni yao, Kamati hiyo ya Bunge jana iliyapitia maoni hayo na kuyajadili kifungu kwa kifungu kwa ajili ya kuboresha muswada huo.

Kamati hiyo ilitakiwa kusikiliza maoni ya wadau hao katika mkutano uliofanyika mjini Dodoma jana, ambapo waliwasilisha barua za kushindwa kuhudhuria kikao hicho na kushauri muswada huo, usogezwe mbele badala ya kuwasilishwa katika Bunge lijalo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema kamati hiyo imepokea baadhi ya barua za wadau hao ambao ni Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), MISA Tan na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) wakiitarifu kamati hiyo kuwa hawatahudhuria wala kutoa maoni yao.

“Kwa mujibu wa barua hizi, wadau hawa wamekiri kupokea mwaliko wetu wa kamati lakini wamesisitiza kuwa hawatohudhuria kwa kuwa wanaamini muswada huo bado unahitaji kusogezwa mbele zaidi,” alisema Serukamba.

Alisema, mapema wiki iliyopita kamati hiyo iliwapatia muda wa takribani siku tisa wadau hao ili waweze kujiandaa na kutoa maoni yenye tija, baada ya kuwasilisha kilio chao kuwa muda waliopewa kupitia muswada huo hautoshi.

“Pamoja na ukweli kuwa muswada unaposomwa kwa mara ya kwanza bungeni unakuwa uko wazi kwa wadau na wananchi, tuliwapatia muda wajipange zaidi kama walivyoomba,”alisisitiza.

Alisema kimsingi kanuni za Bunge, zinabainisha kuwa muswada unaposomwa kwa mara ya kwanza bungeni, kila mwananchi au mdau anayehitaji kuusoma anaupata kirahisi.

“Kwa muda uliosomwa muswada huu Septemba, mwaka huu, wadau hawa walikuwa na muda wa kutosha kuupitia na kutoa maoni yao,” alisema.

Alisema mara baada ya kusomwa kwa muswada huo, si kazi ya Bunge kuwaita wadau na kuwashawishi wausome muswada huo, bali ni utashi wao ndio unaosukuma kuutafuta, kuusoma na kutoa maoni yao kwa Kamati ya Bunge kwa mujibu wa taratibu.

“Kazi yetu sisi Bunge kupitia kamati ni kuwaita wadau watoe maoni yao, ambayo tunayapitia na kujadili na kuyawasilisha kwa Bunge kwa kuishirikisha serikali na kuboresha zaidi muswada,”alifafanua.

Serukamba alisema hiyo si mara ya kwanza kwa wadau wa habari, kuendelea kukwamisha muswada huo usisomwe bungeni, kwani kwa takribani miaka 23 iliyopita, umekuwa ukikwama kuwasilishwa kutokana na migomo ya wadau hao wakiomba muda zaidi.

“Kila mara unapofikia hatua nzuri ya kuwasilishwa bungeni, wadau wanakataa kwa madai kuwa hawako tayari na kuomba usogezwe mbele, sasa wamefanya jambo hili kama ni mchezo. Sasa sisi tunasema kama kukataa kwao kutoa maoni ni njia ya kuonesha wanaukubali lakini wanaficha sura zao au wanaukataa, sisi tutasonga mbele,” alisisitiza.

Mwenyekiti huyo alisema kamati hiyo, kwa sasa inapitia maoni ya wadau wengine, yaliyowasilishwa kwa njia ya barua na barua pepe, ambayo yatajadiliwa na kujumuishwa kwenye mapendekezo ya kamati hiyo kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi.

Hicho ni kikao cha pili cha kamati hiyo cha kukusanya maoni ya wadau, ambapo kikao cha kwanza kilifanyika mapema wiki iliyopita, lakini wadau hao wakiongozwa na Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari (MOAT), walishindwa kuwasilisha maoni na kuomba wapatiwe muda wa miezi minne ili waupitie vyema muswada huo.

Wadau waliohudhuria kikao hicho na kuomba kuongezewa muda ni Jukwaa la Wahariri (TEF), klabu mbalimbali za waandishi wa habari, MCT, MISA-Tan, LHRC na TLS.

Post a Comment

 
Top