Kiungo wa zamani wa Yanga SC na Vancouver Whitecaps ya Canada, Nizar Khalfan anayekipiga Singida United ya daraja la kwanza kwa sasa, ametamba kuwa kwa moto ilionao timu hiyo, lazima ipande ligi kuu msimu ujao na kukabana koo na vigogo wa Tanzania.
Nizar aliyekuwa akikipiga Mwadui FC msimu uliopita, amesema kwa sasa Singida iliyo chini ya kocha msaidizi wa zamani wa Yanga, Fred Felix Minziro, imekaa sawa na ipo tofauti na ya misimu iliyopita katika kila idara, hivyo kilichobaki ni kuzidi kupambana kufika ligi kuu.
Mpaka sasa Singida ndiyo inayoongoza Kundi C la ligi hiyo ikiwa imeshinda michezo minne na kutoa sare mmoja katika jumla ya mechi tano ilizocheza na sasa imesalia michezo miwili kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa kundi hilo.
“Kwa sasa Singida imebadilika na tupo sawa kila idara, ukitazama kuanzia kikosi mpaka benchi limekamilika. Wapo wachezaji wenye uzoefu mkubwa ambao tunasaidiana katika kuipandisha timu, yupo Rashid Gumbo, Razak (Khalfan), Yahya Tumbo na wengine wengi.
“Nafikiri mashabiki waendelee kutusapoti katika hili na kwa pamoja mwisho wa msimu tufanikishe lengo na kutinga ligi kuu na sisi,” alisema Nizar.
Post a Comment