0

Pluijm amejiuzulu pamoja na benchi lake zima na amesema hataki kufanya kazi kama Mkurugenzi wa Ufundi

KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amejiuzulu pamoja na benchi lake zima na amesema hataki kufanya kazi kama Mkurugenzi wa Ufundi.

Amesema hatua hiyo inatokana na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima.

Akizugumza na mwandishi wetu leo, Pluijm amesema kwamba alipaswa kutaarifiwa na uongozi juu ya jambo lolote kuhusu nafasi yake kazini, lakini ajabu anajua kupitia vyombo vya habari.
“Nimejiuzulu na sitafanya kazi tena Yanga. Ninafuatilia haki zangu na baada ya hapo nitaondoka,”alisema. Zaidi Pluijm amekerwa na kitendo cha uongozi kuleta kocha mpya yeye akiwa kazini. “Sijaambiwa chochote. Uongozi umenivunjia heshima sana, kwa klabu kama Yanga SC hawakupaswa kufanya hivyo,”alisema Pluijm.

Aidha, kuhusu uwezekano wa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, Pluijm alisema; “Sipendelei hiyo kazi. Nataka kufanya kazi na wachezaji kila siku kwa matakwa ya moyo wangu. Ninaondoka, mimi ni kocha mkubwa na nina wasifu mzuri. Nitapata timu,”alisema.

Pluijm anaondoka siku mbili kabla ya Yanga kucheza na JKT Ruvu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumatano.
Yanga imerejea leo kutoka Mwanza, ilikopita ikitokea Bukoba, mkoani Kagera ambako Jumamosi ilishinda 6-2 dhidi ya wenyeji Kagera Sugar katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.⁠

Uongozi wa Yanga unamuondoa Pluijm na Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo na kumpa nafasi Mzambia, George Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  

Ikumbukwe, Pluijm yupo katika kipindi cha pili kufundisha Yanga baada ya awali kufundisha kwa nusu msimu mwaka 2014, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts.

Post a Comment

 
Top