0
SUALA la utata wa kimkataba wa kiungo mpya wa Simba, Chichi Mussa Ndusha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limefikishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ili kupatiwa ufumbuzi.


Simba SC imemsajili mchezaji huyo msimu huu, lakini imeshindwa kuanza kumtumia katika mechi za mashindano kutokana na klabu aliyotokea, FC Renaissance kuweka ngumu.


Na klabu hiyo ya DRC inadai bado ina Mkataba naye hivyo imelizuia Shirikisho la Soka DRC kutuma Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) aanze maisha mpya Dar es Salaam.
Simba imefungua kesi FIFA kwa ajili ya kiungo Chichi Mussa Ndusha kutoka DRC 

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda amesema kwamba, kwa sababu hiyo, Simba SC imeamua kufungua kesi FIFA, ikipeleka vielelezo vya kuonyesha mchezaji huyo hana Mkataba na FC Renaissance.


“Kwa kweli niseme tu mustakabali wa mchezaji huyo hadi sasa ni tata. Tunachosubiri ni hiyo Kamati ya FIFA kuketi na kupitia mikataba hiyo na kutoa maamuzi,”amesema Lucas.   


Ndusha ni kati ya wachezaji wapya watano wa kigeni waliosajiliwa msimu huu, wengine wakiwa ni Janvier Bokungu kutoka DRC pia, Method Mwanjali kutoka Zimbabwe, Frederick Blagnon kutoka Ivory Coast na Laudit Mavugo kutoka Burundi. 


Watano hao wote wapya wameungana na wawili kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast na beki Mganda Juuko Murshid waliobaki kutoka kikosi chaa msimu uliopita baada ya kuachwa kwa beki Mrundi Emery Nimubona, kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi na washambuliaji Mganda Hamisi Kiiza, Pape Ndaw kutoka Senegal na Mkenya Paul Kiongera.

Post a Comment

 
Top