|
WIZARA ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imezifuta shule za
awali, msingi na sekondari nchini ambazo hazijasajiliwa zaidi ya 40
kuanzia Julai mwaka jana.
Awali
kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, waligundua kuwepo kwa shule 35
zisizosajiliwa na kuzifuta, jambo lililofanya kutangaza shule zote
ambazo hazijasajiliwa kujisalimisha ili kusajiliwa.
Kaimu
Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika wizara hiyo, Khadija Mcheka
alisema Mei mwaka huu baada kuzipa miezi miwili shule ambazo
hazijasajiliwa kufanya hivyo, walizifungia shule nyingine 12.
Mcheka
alisema shule zinaweza kufutwa kwa sababu mbili zikiwamo zilizosajiliwa,
lakini zikakiuka vigezo ambazo zikitimiza vigezo zinaweza kuomba upya
usajili na kupewa.
“Lakini
aina ya pili ni zile ambazo hazijasajiliwa na zinaendeshwa kinyume cha
sheria ambazo nazo zikifuata taratibu zikatimiza vigezo zinaweza kupewa
usajili,” alifafanua Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule.
Alisema
katika kipindi hicho mpaka Agosti mwaka huu baada ya tangazo la kuwataka
kusajiliwa shule za awali nne, zile za awali na msingi 105 na sekondari
19, walifika wizarani kwa ajili ya kupata taratibu za usajili ambapo
zipo zilizosajiliwa na nyingine kupewa vibali.
Alisema
katika usajili, kuna wapo waliokidhi viwango na wengine waliopatiwa
maelekezo na kupatiwa vibali vya kutumia majengo yaliyopo huku wengine
wakipewa vibali vya kujenga majengo ya shule kabla ya kupata usajili.
Alisema
kwa shule walizozifungia, waliwaandikia barua za kuwafungia na kuwataka
kuhakikisha wanawatawanya wanafunzi katika shule zilizosajiliwa kwa
gharama zao bila kuwaathiri wanafunzi.
Alitaja
shule zilizofungiwa kwa kuendesha shughuli zake bila usajili kuwa ni
shule za awali na msingi za Must Lead ya mkoa wa Pwani, na za mkoa wa
Dar es Salaam ni Brainstorm, Pax, Lassana, Grace, Rose Land, Julius
Raymod, St Thomas, Mary Mother of Mercy, Noble Sinkonde, Immaculate
Heart of Mary, St Columba, Corner stone, Dancraig, Mwalimu Edward
Kalunga, Edson Mwidunda, Gisela, Kingstar, St Columba awali, Bilal
Muslim, Thado, Hocet , Elishadai, Lawrance Citizen, Comrade, Dar Elite
Preparatory na Golden Hill Academy na Hekima.
Nyingine
ni Pwani Islamic, St Kizito na Rwazi Encysloped za Kagera, Dancraig na
Qunu za Pwani, Hellen’s ya Njombe, Joseph ya Arusha, Samandito na Maguzu
za Geita. Alizitaja shule za Sekondari zilizofungiwa kwa sababu hiyo
kuwa ni Hananasif, Elu, Hocet, Safina za Dar es Salaam na Namnyaki ya
Iringa.
Aidha, Shule ya Fountain Gate ya jijini Dar es Salaam imefungiwa kwa kuendesha bweni bila kibali.
“Baada ya
kutoa tangazo kutokana na kubaini kuwapo shule nyingi zisizosajiliwa,
wapo waliojitokeza na nyingine tumezifungia kutokana na kutokidhi
viwango vya usajili lakini pia tunaamini wapo waliojificha wakiendelea
kutoa huduma,” alisema Mcheka na kuwaagiza wakaguzi katika kanda na
wilaya, kufanya ukaguzi na kutoa taarifa kwa zile ambazo hazijafungiwa
na ikithibitika hazijasajiliwa, kuzifungia mara moja.
Alisema
utaratibu uliopo kwa kuhakikisha shule zote zinasajiliwa kulingana na
viwango stahili kwa lengo la kutoa elimu bora ni wakaguzi wa kanda,
mikoa na wilaya kwa kushauriana na waratibu wa elimu katika kata,
kuhakikisha shule yoyote inayochomoza, wanaifuatilia na kuwapa ushauri
wa kufuata taratibu za usajili kwa kukidhi viwango stahili.
Alisema
wamekuwa wakigundua kuwapo kwa shule, ambazo hazijasajiliwa kutokana na
wakati wa mitihani idadi ya wanafunzi inazidi tofauti na walivyosajiliwa
na kubainika kuwa wapo waliokuwa wakisoma katika shule, ambazo
hazijasajiliwa wanawapeleka katika shule zilizosajiliwa.
“Kuna
wenye shule ambazo hazijasajiliwa wakati wa mitihani wanakuja kuomba
wanafunzi kufanya mitihani hivyo kuleta usumbufu wa kuwatawanya kwenye
shule zilizosajiliwa na kwenda kuwakagua ili kuweza kusajiliwa,”
alifafanua.
Msajili
huyo alisema madhara yanayotokana na mwanafunzi kusoma shule ambazo
hazijasajiliwa ni pamoja na haitajulikana mtoto anachosoma kwani
haitajulikana mitaala wanayotumia kutokana na kukosa usajili, hivyo
kushindwa kufanya mitihani. Pia mazingira ya shule na mpangilio wake,
haitaendana na matakwa ya serikali ya kutoa elimu bora kwani mmiliki
atafanya kile anachotaka.
Mei mwaka
huu, wizara hiyo ilizipa miezi miwili hadi Julai 30, mwaka huu
kuhakikisha shule zote ambazo hazijasajiliwa zinajisajili kabla ya
serikali kuzifunga.
Kaimu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Leonard Akwilapo alisema ifikapo Julai 30, mwaka huu, mmiliki
wa shule itakayobainika kutosajiliwa ikiwemo zitakazokosa vigezo vya
kusajiliwa, atapaswa kuhamisha wanafunzi waliopo kwa gharama zake.
Alipoulizwa
ni shule ngapi ambazo zinajiendesha bila kusajiliwa, Kaimu Mkurugenzi
Mcheka alisema tatizo kubwa lipo kwa shule za awali na msingi.
Post a Comment