BARAZA la
Taifa la Uwezeshaji limesema fedha Sh milioni 50 za kila kijiji
zilizoahidiwa na Rais John Magufuli, utaratibu wa utoaji wake
unaandaliwa na mapema mwanzoni mwa mwaka ujao zitakuwa zimetoka.
Mkurugenzi
wa Mifuko ya Uwezeshaji katika Baraza hilo, Edwin Chrisant ameyasema
hayo jana jijini Dar es Salaam katika juma la benki za maendeleo vijijini
(Vicoba) na kuongeza kuwa fedha hizo zitakwenda kwa wananchi walioko
katika vikundi peke yake.
Maadhimisho
hayo ya Vicoba yameandaliwa na Asasi iliyo ya kiserikali ya kijamii ya
Maendeleo na Uchumi inayojishughulisha kutoa elimu na mafunzo kwa
wanachama wa vyama hivyo (SEDIT).
Kuhusu
fedha hizo za ahadi za Rais Magufuli, mkurugenzi huyo alisema serikali
itakamilisha mpango wa fedha hizo kwa kila kijiji na zitakwenda kwa wale
walioelimishwa namna nzuri na utaratibu wa fedha ili zifanye kazi
iliyokusudiwa.
Alisema
utoaji wa fedha hizo kwa kipindi hicho utakuwa wa aina tofauti na
zitahakikishwa zinawafikia wananchi wa kipato cha chini kwa masharti
yaliyo rahisi, ikiwa ni pamoja na kuwatambua zaidi walioko katika
vikundi.
Alisema
Watanzania wenye dira ya shughuli za kiuchumi suluhu ya kufikia malengo
yao ni kupata mtaji, jambo ambalo Baraza la Uwezeshaji linashughulika
nalo ili kupanua wigo wa maendeleo nchini.
Mkurugenzi
wa SEDIT, George Sweveta alisema taasisi zinazotoa elimu kwa Vicoba
zimepata sera mpya ambapo muda wowote wanaweza kupata sheria ambayo
inaweza kuwalinda na kuwawezesha kukaa meza moja na serikali kwa ajili
ya maendeleo ya vyama hivyo.
Post a Comment