0

VIONGOZI wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, wamemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad akae pembeni kama ameshindwa kuongoza chama hicho.

Walisema hayo wakati wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Mpilipili kata ya Ugunda wilayani humo.

Walisema hawatambui maamuzi ya kusimamishwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya.

Mwenyekiti wa CUF wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya kitongoji cha Mpilipili, Lubaga Lubaga, alisema wao kama wilaya bado wanawatambua viongozi hao.

Lubaga alibainisha kuwa kinachofanyika ndani ya chama hicho kwa sasa ni usanii wa Maalim Seif, hivyo wakiwa kama wanachama halali wa chama hicho Kaliua wataendelea kupingana naye.

“Maalim Seif kwanza hana msaada wowote kwani hata alipokuwa kwenye serikali ya mseto iliyopita visiwani Zanzibar hakuwa na msaada wowote na mkoa wa Tabora, hivyo kama ameshindwa kuongoza CUF akae pembeni,” alisisitiza Lubaga.

Alisema hawajaona kosa lolote alilofanya mbunge wao, Sakaya.

Alisisitiza wao bado wanamtambua Sakaya kuwa ni mwakilishi wao bungeni.

Kuhusu maamuzi ya kumteua Julius Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa muda wa CUF, alisema hatua hiyo ni kukiuka Katiba ya chama chao na inaonesha dhahiri kuwa sasa ndani ya chama hicho, kuna mchezo mchafu unaofanywa kwa maslahi ya watu wachache.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Tuombe Mungu, Abdulrahaman Toni alisema CUF wilaya ya Kaliua, bado wako imara na wanawaunga mkono Profesa Lipumba na Sakaya, hivyo maamuzi yaliyofanywa dhidi ya viongozi hao ni batili.

Post a Comment

 
Top