HOSPITALI
ya kisasa ya kufundishia wataalamu wa afya na kutoa huduma ya Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyopo eneo la
kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kufunguliwa
rasmi na kuanza kutoa huduma Januari mwakani.
Hospitali
hiyo iliyojengwa kisasa kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (Tehama), itakuwa ya kwanza kutumia mfumo wa
teknolojia ya sampuli hewa, unaochukua vipimo kwa mtambo maalumu na
kuwasilisha majibu kwa njia ya mtandao na itakuwa na wadi ya watu
mashuhuri akiwemo Rais.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika ziara maalumu katika jengo hilo
lililokamilika ujenzi wake tangu Agosti mwaka huu, Makamu Mkuu wa Chuo
cha MUHAS, Profesa Ephata Kaaya, alisema hospitali hiyo, itatoa tiba ya
magonjwa yakiwemo sugu kama vile moyo, saratani na figo.
Alisema
hospitali hiyo, imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya
dijitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za
X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalumu kwa ajili ya kupimia magonjwa ya
wanawake, mashine maalumu za kupima na kutibu meno, koo, masikio na pua.
“Pia
tumefunga mtambo wa kisasa zaidi wa sampuli hewa uliopo katika kila
idara na kuunganishwa na maabara ambao kazi yake ni kusafirisha vipimo
na kupeleka sehemu mbalimbali na majibu ya vipimo hivyo huwasilishwa
sehemu husika kwa njia ya mtandao,” alisema.
Alisema
mtambo huo, unasaidia kupunguza tatizo la msongamano katika chumba cha
maabara, unaongeza ufanisi na usahihi wa vipimo lakini pia hupunguza
muda na kuepusha mkanganyiko wa vipimo. Profesa Kaaya alisema hospitali
hiyo pia itatoa huduma za kufundishia, kufanya uchunguzi wa magonjwa
mbalimbali na tafiti za fani za afya.
“Lakini
pia tuna vyumba maalumu 12 kwa ajili ya wagonjwa wenye magonjwa
ambukizi kama vile ebola, kipindupindu na kifua kikuu,” alisema.
Alisema
jengo la hospitali hiyo lina ghorofa tisa ambazo zinajumuisha vyumba 13
vya upasuaji kikiwemo chumba kimoja cha upasuaji kwa wagonjwa wa
dharura, maabara za kisasa, vyumba vya wagonjwa mahtuti na kusafisha
figo, wodi za kujifungulia, chumba cha kuhifadhi maiti na vyumba vya
kufundishia.
Aidha
alisema katika eneo la wodi zipo wodi 12 za wagonjwa mashuhuri vikiwemo
vyumba viwili vyenye mitambo ya kisasa ya kufuatilia hali ya mgonjwa
vya viongozi wenye hadhi ya juu akiwemo Rais.
Profesa
Kaaya, alisema ujenzi wa hospitali hiyo uliogharimu kiasi cha dola za
Marekani milioni 94.5 katika eneo hilo la Mloganzila lenye ukubwa wa
ekari 3,800, ulianza tangu mwaka 2014 kupitia mkopo wenye riba nafuu
ambao malipo yake yataanza kulipwa baada ya miaka 15 kwa kipindi cha
miaka 25.
Kwa
mujibu wa Profesa Kaaya, hospitali hiyo itakayokuwa pia ya rufaa,
itasaidia kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wenye magonjwa sugu kwenda
nje ya nchi kutibiwa kwani itatoa tiba na vipimo vya magonjwa mengi sugu
yanayosumbua Watanzania.
|
Post a Comment