Alfajiri ya Jumamosi, 30 Desemba 2006 muda mfupi kabla ya saa 12:00,
itakuwa siku ya kukumbukwa katika historia ya taifa la Iraq, kwa
machungu au kwa furaha miongoni mwa wananchi wa taifa hilo kutokana na
kunyongwa kwa aliyekuwa mtawala wa taifa hilo aliyeondolewa madarakani
na majeshi ya kimataifa yakiongozwa na Marekani na Uingereza.
Saddam Hussein Abd al-Majid al-Tikriti, ambaye alikuwa mtawala wa taifa
la Iraq amekabiliwa na changamoto ya msemo huo kufuatia kutekelezwa kwa
hukumu iliyotolewa na mahakama moja nchini Iraq ya ‘kunyongwa hadi kufa’
baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kibinadamu uliomkabili licha
ya kukata rufaa na ktupwa baadaye.
Wengi tulizoea kusikia majina yake ya Saddam Hussein, lakini majina yake
halisi ni kama yalivyotajwa hapo juu na alizaliwa tarehe 28, Aprili
mwaka 1937 katika kijiji cha Tikrit katikati ya Iraq, na aliingia
madarakani tarehe 16 Julai 1979 na kulitawala taifa hilo kwa mkono wa
chuma hadi tarehe 9 Aprili 2003 alipoondolewa kwa nguvu na majeshi hayo.
Hukumu hiyo ambayo inatia simanzi na furaha kwa pamoja kulingana na
mitazamo ya watu kuhusiana na sakata la kuibuka na kuporomoka kwa Saddam
imetekelezwa kwa wakati kama alivyoahidi Waziri Mkuu wa nchi hiyo,
Nouri al-Malik, kwamba hukumu dhidi ya kiongozi huyo itatekelezwa kabla
ya mwisho wa mwaka huu.
Kuuawa au kunyongwa kwa Saddam imekuja kufuatia hukumu iliyotolewa na
Mahakama Maalum iliyomtia hatiani kwa mauaji ya wanakijiji waarabu wa
madhehebu ya Shia wapatao 150 baada ya kushindwa kwa jaribio la kumuua
mwaka 1982.
Pia akikabiliwa na mashitaka mengine ya mauaji ya kimbari dhidi ya
Wakurdi 180,000 wengi wao wakiwa raia wa Iraq mwishoni mwa miaka ya
1980.
Kiongozi huyo aliyeitawala Iraq kama rais wa tano wa nchi hiyo
alionekana akiwa na amebeba kitabu kitukufu cha Koran huku akisema kwa
sauti kuu kuwa 'hakuna Mungu mwingine bali Allah na Muhammad ni Mtume
wake', alinyongwa katika kasri ya wizara ya Sheria.
Kufuatia kifo hicho habari zinaeleza kuwa katika jiji la Washia la Sadr
karibu na Baghdad, watu wameonekana wakicheza na kushangilia mwisho wa
maisha ya Saddam, huku kusini mwa jiji la Baghdad mlipuko wa bomu
umewaua watu wapatao 30 katika soko la samaki.
Mwezi Oktoba, 1959 alihusika katika jaribio lililoshindikana la kumuua
mtawala wa Iraq kipindi hicho, Jenerali Abdul Karim Qassem, na
kukimbilia uhamishoni katika nchi ya Misri alikoishi kwa miaka minne.
Saddam alirejea Baghdad Februari, 1963 na kujiunga na chama cha Baath
kilichoingia madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kuondolewa
madarakani miezi tisa baadaye, na viongozi wa chama hicho kutupwa
gerezani.
Hata hivyo alichaguliwa kuwa Makamu Katibu Mkuu wa chama hicho akiwa
gerezani huku wenzake wakiendeleza harakati za mapinduzi ambayo
yalifanikiwa miaka mitano baadaye.
Akiwa mwanachama na kiongozi wa chama cha Baath Arab Social Party
kilichofuata sera za ujamaa wa kiarabu na uchumi ulioendelea, Saddam
alichukua jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba anastawisha maisha ya
wananchi wake huku akikazana kuleta mapinduzi ya kiuchumi miongoni mwa
mataifa yaliyoko kwenye jumuiya ya kiarabu.
Saddam ambaye ameacha wajane watatu; Sajida Talfah, Nidal al-Hamdani na
Samira Shahbandar alikuwa miongoni mwa viongozi wa mstari wa mbele
katika mapinduzi yaliyokiweka chama chake madarakani Julai 1968 baada ya
kumuondoa madarakani, Abdul Mohamed Aref, na kukiwezesha kutawala Iraq
kwa kipindi kirefu.
Akiwa Makamu wa Rais chini ya uongozi wa mpwa wake, Jenerali Ahmed
Hassan al-Bakr, Saddam aliongoza na kuendekeza chokochoko baina ya
utawala na viongozi wa kijeshi katika utawala huo na kuimarisha wapambe
wake katika safu ya uongozi na usalama kwenye kada ya utawala kwa lengo
la kudhoofisha uongozi wa kijeshi.
Wakati rais wa nne wa Iraq, Jenerali Hassan al-Bark akijihusisha na kazi
ya kutaifisha kampuni kubwa ya uchimbaji mafuta ya Iraq Petroleum
Company na kuyalipa makampuni mengine ya kigeni na kuyaondoa nchini,
Saddam alikuwa akijikita katika kufanya kazi ya kuhakikisha kuwa
anaendelea kujijenga katika uongozi wa Iraq.
Utawala wa Baath ulikabiliwa na upinzani kutoka kwa Wakurdi ambao
waliendeleza chokochoko dhidi ya utawala wa Baghdad na kupelekea
kusainiwa kwa kwa mkataba wa mpaka baina ya Iraq na kiongozi wa kidini
wa Iran, Shah mwezi Machi 1975; ingawaje Shah huyo aligeuka na kuendelea
kuwapa misaada wakurdi hao.
Kiongozi wa Iraq, Jenerali Hassan al-Bark, alilazimika kustaafu kwa
kilichoelezwa kuwa na umri mkubwa mwezi Julai 1979 na Saddam ambaye
alikuwa muislamu wa madhehebu ya Sunni alichukua uongozi wa taifa hilo
ingawaje wadadisi wa mambo ya kisiasa wanadai kuwa Jenerali huyo
alilazimika kustaafu kufuatia saddam kujiimarisha na kuchukua uongozi
usio rasmi wa taifa.
Ghasia zilizoendelezwa na Wakurdi katika mpaka wa Iran na Iraq
ilipelekea kuanza kwa vita vilivyodumu kwa miaka minane kati ya Iran na
Iraq, mwezi Septemba 1980.
Iraq ambayo imetokea kuwa wahasimu wakubwa wa Marekani, katika vita
hivyo ilikuwa ikisaidiwa na taifa hilo kubwa duniani dhidi ya Iran
katika vita vilivyogharimu maisha ya watu wapatao milioni moja .
Alipigana vita hivi kwa lengo la kuondoa tishio la kikabila na kidini
lililokuwa likiukabili utawala wake kutoka kwa makundi yaliyokuwa
yakitaka kujitawala au kupewa uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe
ndani ya mipaka ya kikabila na kidini nchini Iraq.
Wakati wa vita hivyo, Saddam alijulikana kama shujaa pekee wa Kisunni
aliyesimama kidete dhidi ya wahasimu wa Marekani na Israel katika
jumuiya ya kiarabu na hii ilimjengea heshima mbele ya mataifa hayo
ambayo yalikuja kumgeuka baadaye kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa amani
mwezi Agosti, 1988 kati yake na Iran.
Katika vita hivyo, kiongozi huyo wa Iraq alijivunia nguvu za maaskari
wake 190,000, vifaru 4,500, magari ya kivita4,000, ndege za kivita 500
na helikopta 400 dhidi ya Iran ambayo ilikuwa na nguvu za wanajeshi
305,000, wanamgambo 500,000, vifaru 1,000, ndege za kivita 65 na
helikopta720.
Ingawaje chaguzi kadhaa za urais zimeendeshwa kipindi cha utawala wake,
Saddam aliwachukulia hatua kali na za mateso watu wote walionyesha
kuupinga utawala wake, waliokataa kupiga kura au waliopiga kura za
kumpinga.
Urafiki wa iraq na Marekani uliingia nyongo pale alipojaribu kutikisa
nguvu za taifa hilo kwa kuivamia nchi ya Kuwait mwezi Agosti 1990 na
kupelekea Marekani kuendesha vita vilivyojulikana kama 'Operation Desert
Storm' dhidi ya uvamizi huo.
Katika kuuonyesha ulimwengu kuwa ana nguvu katika nchi yake, Saddam
aliitisha uchaguzi nchini humo na kubuka kidedea kwa kupata zaidi ya
asilimia 99 za kura zote na Oktoba mwaka 2002 akajinyakulia asilimia 100
za kura katika uchaguzi mwingine wa urais nchini Iraq.
Baada ya kujijengea uadui na Marekani na mshirika wake Israel, Marekani
iliendeleza chokochoko dhidi ya utawala wa Iraq ikidai kuwa nchi hiyo
ina akiba kubwa za kemikali na silaha za nyuklia na hivyo kuihusisha na
kundi la magaidi la al-Qaeda la Osama bin Laden.
Madai hayo hata hivyo yalikanushwa vikali na Saddam mwezi Februari, 2003
lakini ilipofika tarehe 20 mwezi Machi 2003, Muungano wa mataifa kadhaa
ukiongozwa na Marekani uliivamia Iraq kinyume cha azimio la Umoja wa
kimataifa (UNO) lililokataa kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
Aprili 9, 2003 majeshi ya marekani yalifika katika jiji la Baghdad na
kuwaua watoto wa Saddam; Uday na Qusay Hussein baada ya kushambulia
makazi yao kwenye mji wa Mosul Julai 22.
Mtawala huyo alikwenda mafichoni kuepuka kukamatwa na majeshi ya
Marekani na washirika wake lakini juhudi za kukwepa mkono wa majeshi
hayo hazikuzaa matunda kwani ilipofika tarehe 13 desemba 2003 alitiwa
mbaroni na kukamatwa kwake kukatangazwa rasmi.
Tarehe 19 Oktoba 2005, Saddam alifikishwa mbele ya mahakama maalum
kusikiliza mashitaka ya mauaji ya 1982 ya washia 150 katika mji wa Dujal
baada ya jaribio lao la kumpindua kushindikana na Agosti 21, 2006
mahakama ikaanza kusikiliza mashitaka mengine ya mauaji ya maelfu ya
Wakurdi 1988.
Majaji wa mahakama hiyo waliteuliwa na Baraza linalotawala nchini Iraq
kwa kushauriana na Baraza la Sheria na kupewa kazi kwa miaka mitano
likiongozwa na Jaji Rizgar Mohamed Amin akisaidiwa na Rauf RashidAbd
al-Rahman na wengine.
Mahakama hiyo ilimkuta saddam na hatia ya makosa dhidi ya Ubinadamu
tarehe 5 septemba 2006 na kumhukumu kunyongwa, hukumu ambayo aliikatia
rufaa ingawaje Mahakama Kuu ya Rufani ya Iraq iliitupilia mbali rufani
yake 26 Desemba 2006 na kushikilia hukumu ya kunyongwa, zoezi ambalo
limetekelezwa na kuhitimisha historia ya Saddam Hussein.
Post a Comment