0
bills-invoices-writing-signing-first-of-month
Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaojitetea kwa namna moja au nyingine kuwa hawana haja ya kuwa na malengo katika maisha yao kwa sababu ya kufikiri wana kila kitu au wana muda wa kutosha wa kupanga badae au wanazani wana nafasi kubwa ya kufanya hivyo huko mbele, basi hadi sasa umekosea kuwaza na kwa namna hiyo jiandae kufeli na kushindwa kabisa katika mambo mengi ambayo unafikiri utayafanya na kufanikiwa kama mchezo wa bahati nasibu. Kama unahitaji kuyafanya maisha yako yawe kwenye mpangilio unaoeleweka na kutimiza majukumu yako vizuri ya kila siku hauna budi kuwa na malengo yanayoweza kukuongoza kufikia mahali unapotaka kwenda ili kutimiza ndoto ya maisha yako.
Malengo ni hatua, malengo ni mtiririko wa mawazo mengi uliyonayo kwa ajili ya maisha yako ya badae. Angalia ni mambo mangapi leo hii unayahitaji yatimie katika maisha yako, angalia leo hii ni mambo mangapi unayotamani yafanikiwe ili kuleta matokeo chanya katika eneo fulani la maisha yako. Yawezekana kila unapokaa mwenyewe unakuwa una mawazo fulani au maswali mengi kama vile, “ningefanikiwa kufanya biashara kipindi kile nilichokataa naamini leo hii ningekuwa mbali kama fulani; kama nikianzisha mradi huu wa kuku kufikia mwakani si nitakuwa mbali sana kwa kuuza mayai yake; hivi nikiamua kurudi shule kusoma si utakuwa ni uamuzi mwema sana wa kunisaidia kuongeza ujuzi ili nipandishwe cheo; sijui nianze kuweka akiba na kuwekeza katika soko la hisa ili niongeze mtaji katika biashara yangu.”
Kwa nini uimbe na kuwaza tu pasipo kupanga na kujiwekea malengo? Hayo ni baadhi ya maswali na mtiririko mawazo machache kati ya mengi ambayo kila mtu anaweza kukutana nayo ya aina hiyo, hasa pale anapokuwa na nafasi ya kukaa na kutafakari mwenyewe juu ya maisha yake ya badae. Hebu fikiri kila mwaka unasema “natamani au ningefanya au sijui nifanye au sijui nianze kufanya, nakadhalika.” Angalia ni muda gani na miaka mingapi utabaki ukiimba wimbo wa kutamani kuwa na maisha fulani mazuri unayoyaona kwenye akili yako au kwa wengine, huku wewe mwenyewe binafsi hutaki kuchukua hatua ya kupanga kwa ajili ya maisha yako hayo. Kwa nini uimbe na kuwaza tu pasipo kupanga na kujiwekea malengo?
Huwezi kubaki unatamani; unahitaji kutoka kwenye viwango au level ya kutamani (ku- wish) na kuamua kupanga kwa ajili ya maisha yako (plan for your future). Mafanikio yako utayaona pale unapoona umetimiza jambo fulani kubwa ulilokuwa ukilihitaji kwa muda mrefu katika maisha yako, na hicho ndio chanzo cha furaha na kusonga mbele zaidi. Na kumbuka ili uweze kuona mafanikio halisi unahitaji kuweka malengo, lakini pia unahitaji kuweka mikakati imara ya kukusaidia kufikia mahali unapotaka kuwa kwenye maisha yako ya badae. Hebu jiulize unataka kuwa wapi baada ya miaka mitano kutokea sasa na nini kifanyike ili uweze kufikia hapo? Unaona picha gani mbele yako kwenye miaka mitano kutokea sasa? Unajiona wapi kiuchumi, kiafya, kiufahamu au elimu, mahusiano na wengine, familia, nakadhalika? Kama hauna picha yoyote ya maisha yako ya badae kwa nini hadi sasa unalalamika maisha ni magumu.
Kumbuka leo hii unalalamika maisha ni magumu ni kwa sababu ya uamuzi wako wa kutokupanga huko nyuma kama ambavyo huchukui hatua ya kupanga hivi leo. Unahitaji kupanga leo ili kurahisisha hatua za maisha yako utakapoifikia hiyo kesho. Usiishi maisha ya kutegemea kwamba kuna siku moja utafanikiwa tu tena labda kwa bahati, kwamba utalala na kuamka tajiri kama Bakhresa au Bill gate na wengineo. Hakuna kitu kama hicho chini ya jua, bali fahamu hata hao unaowaona leo hii ni matajiri na mabilionea wakubwa duniani wamefikia hapo walipo ni kwa sababu waliyapangilia na kuyachora (design) maisha yao ya leo miaka mingi nyuma kabla hatujafikia kuwaona hapo walipo na kuwatamani.
Unahitaji kuweka malengo ili uweze kuyafanya maisha yako kuwa ya kipekee hapa duniani na ili uweze kuifikia ndoto yako ya maisha uliyonayo. Brian Tracy ambaye ni msemaji na muhamasishaji wa maendeleo ya mtu binafsi nchini marekani anasema kuwa, “I discovered goals and was never the same again.” (Nilipogundua malengo sikuwa mtu wa kawaida tena). Nataka nikuambie hata wewe unahitaji siku moja kuzungumza lugha ya namna hiyo, kwani hadi Brian Tracy kuzungumza lugha ya namna hiyo ana maana na ameona matokeo makubwa baada ya kuwa na tabia ya kujiwekea malengo kwenye maisha yake.
Historia ya Brian Tracy aliyoitoa yeye mwenyewe binafsi inaonyesha kuwa, alikuwa ni mtu mwenye kuosha vyombo kwenye hotel na migahawa alipokuwa kijana, tena hakuwa na elimu kubwa kama wengi wanavyoikiri zaidi ya ufahamu wa kufanya mauzo alioupata hapo badae. Ila baada ya kujifunza zaidi na zaidi na kuelewa umuhimu wa kusoma vitabu kila siku, ndipo alipokutana na ujuzi wa pekee wa kujiwekea malengo na mkakati kwa ajili ya kuboresha na kufanikiwa maishani mwake. Hadi sasa ni mmoja wa wahamasishaji wakubwa duniani na ni msemaji anayesimama miongoni mwa maelfu ya watu nchi hadi nchi duniani kote kwa ajili ya kuwasaidia watu kufikia ndoto na malengo yao, na pia ni mwandishi wa vitabu vingi sana vilivyouza na kuteka soko la vitabu ulimwenguni kote.
Nataka nikupe siri hii kuwa, malengo ni kama mafuta kwenye gari yako, huwezi kuendesha gari huku unajua hauna mafuta ya kukufikisha unapotaka kwenda. Mtu hasiye na malengo ni kama meli isiyokuwa na rada ya kuiongoza inapokwenda, kwa njia hiyo tambua meli hiyo itakuwa hatarini na inaweza kugonga mwamba na kuzama mara moja. Mtu mwenye malengo Brian Tracy anamfananisha na kapteni wa meli anayeongoza meli yake yenye kila kitu kama vile rada, ramani ya kumwongoza kule anapokwenda ili aweze kufika mwisho mwema wa safari yake aliyoichagua yeye mwenyewe binafsi.
Hebu jiulize wewe mwenyewe binafsi una malengo gani muda huu yanayokuongoza kwa mwaka huu, mwezi huu, au kila wiki na kila siku kwa ajili ya kuufikia mwisho mwema wa maisha yako na kutimiza ndoto yako na kusudi la Mungu alilokuitia hapa duniani. Emilian Busara mwalimu wa masuala ya fedha na uwekezaji hapa nchini kwetu Tanzania amewahi kuzungumzia suala hili kwenye moja ya vitabu vyake akisema, “jambo baya ambalo watu wengi wanalifanya ni kuzani wanao muda wa kutosha kwa ajili ya kupanga kesho na kuacha kupanga leo, hili ni jambo dogo ila limeendelea kuleteleza umasikini kwa wengi.” Angalia ni hali gani uliyokuwa ukitamani kuachana nayo na kuiepukana nayo katika maisha yako lakini hadi sasa umeendelea kujitia moyo kuishi katika hali hiyo, huku ukweli ni kwamba hauhitaji kuwa kwenye hali hiyo hadi hivi sasa, hii ni kwa sababu hautaki kuchukua hatua ya kupanga kwa ajili ya maisha yako ili uondokane na hali hiyo. Angalia ni mara ngapi umeshindwa kutimiza wajibu wako ulionao hapo kazini kutokana na mlundikano wa kazi nyingi, na hivyo kushindwa kufanya hata mojawapo ya kazi na kuishia kulalamikiwa na bosi wako. Huna muda wa kupanga na kuweka malengo yako ya kazi hiyo ndio sababu.
Kila siku unalalamika juu ya umasikini; unalalamika juu ya faida kidogo unayoipata katika biashara yako; unalalamika mshahara ni mdogo huku ndugu wanakutegemea; unalalamika hupandishwi cheo kazini kwako; unalalamika matokeo ya mitihani ni mabaya; unalalamika unapoteza fedha zako haujui zinatumika kwa jambo gani, huku mmiliki ni wewe; unalalamika hupati tunzo tangu umeaanza kuimba; Nataka nikuambie huwezi kuona matokeo chanya yoyote kama unavyotaka maishani mwako kama hutaki kuchukua hatua kamilifu ya kuamua kuweka malengo yako leo hii na kupanga mkakati wa kufikia hapo unapopataka. Amua leo hii kujiwekea malengo yako pasipo kusubiri kufanya zoezi hilo kesho, ili uweze kuleta matokeo chanya na makubwa juu ya ndoto yako.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO

Post a Comment

 
Top