Prof. Ibrahim Lipumba
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi CUF, Prof Ibrahim Lipumba amesema yeye ndiye mwenyekiti halali
wa chama hicho licha ya Baraza Kuu la chama hicho kutangaza kumsimamisha
uanachama, yeye na wenzake 10.
Lipumba
amesema kikao kilichokaa jana visiwani Zanzibar na kufanya maamuzi ya
kuwasimamisha uanachama, hakikuwa halali na kilikuwa nje ya katiba ya
CUF, sababu mojawapo ikiwa ni kuwekwa kando kwa Naibu Katibu Mkuu Bara,
Magdalena Sakaya.
"Hicho kikao hakikuwa halali, haiwezekani Baraza Kuu linakaa halafu
Naibu Katibuy Mkuu Bara hajui, wala hakujulishwa, na bado kuna wajumbe
wengine hawakuhusishwa" Amesema Prof Lipumba
Lipumba amesema ni kweli alijiuzulu uenyekiti, lakini baadaye aliamua
kuandika barua kwa Katibu Mkuu ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na
sasa yeye ndiye Mwenyekiti wa chama hicho.
"Nilimuandikia barua ya kurudi kwenye nafasi yangu, akasema anasubiri
ushauri wa kisheria, lakini hadi sasa hakuna kitu, hiyo inamaanisha
kuwa sasa mimi naendelea na nafasi yangu, na niko ngangari kama
mwenyekiti" Amesema Prof Lipumba.
Amesema alitaka kujieleza katika mkutano mkuu mbele ya wanachama, lakini mkutano ule ukavurugwa.
Kuhusu kuwepo kwa tofauti kati yake na Katibu Mkuu wa chama hicho
Maalim Seif Sharif Hamad, Prof Lipumba amesema kuwa huenda kuna tofauti
kwa kuwa mara nyingi huwa hamuelewi jinsi anavyokiendesha chama bila
kifuata misingi ya kidemokrasia.
"Katibu Mkuu anamdharau na hampi heshima yake Naibu Katibu Mkuu Bara,
mara nyingi huamua mambo yake bila kushirikisha viongozi wengine,
halafu sasa anataka kufukuza wanachama, huwezi kuwa na chama halafu
ufukuze wanachama, wanachama wanatafutwa duniani kote, halafu wewe
unawafukuza, hizo ni dalili za uongozi wa kiimla, kuongoza chama
unapaswa kujali demokrasia na siyo kuwa dikteta ndani ya chama" Amesema
Kuhusu Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uongozi,
Lipumba amesema kuwa hatambui maamuzi hayo, na wala hamtambui Mtatiro
kama kiongozi wa chama hicho bali mjumbe wa Mkutano Mkuu, nafasi ambayo
yeye ndiye aliyempa.
"Mtatiro hawezi kuwa mwenyekiti, mimi ndiye mwenyekiti wa chama,
Mtatiro alishindwa hata kuongoza mkutano mkuu, ukavurugika, hawezi,
simtambui"
Post a Comment