MSOMI
maarufu nchini, Profesa Benson Bana na mwanasiasa aliyekuwa Makamu
Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, Leticia Mosore wamesema maandamano
yaliyopewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta),
hayawezekani kwani ni ndoto ya mchana na hayana msingi wowote wala tija
kwa wahusika hata kwa Taifa.
Aidha,
maandamano hayo ya nchi nzima imeelezwa kuwa ndio kifo cha Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwani kila chama kimekuwa kikihangaika
kivyake.
“Wanaotaka
kuandamana wanajidanganya na kuwalaghai wenzao kwani kufanya operesheni
ni suala la dola na si la mtu au kikundi cha watu, hivyo maandamano
hayo hayawezekani kabisa,” alisema Profesa Bana katika mahojiano maalumu
na Idara ya Habari (MAELEZO).
Mhadhiri
huyo Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliongeza kuwa
wanaojiita Ukuta ni kwamba Rais John Magufuli amewanyima ajenda, kwani
utendaji wake umezidi fahamu zao na kuwafanya waanze kutapatapa wasijue
nini cha kufanya.
Alisema
kama viongozi wa Ukuta ni waungwana, inabidi watamke wazi kuwa
wametafakari na kuona kuwa maandamano hayana maana hivyo wameamua
kuyasitisha nchi nzima.
Kuhusu
utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, Profesa Bana alisema ni serikali
yenye maamuzi ya uhakika na inayowajali watu wote bila kujali itikadi
zao za vyama, dini wala makabila hivyo inabidi Watanzania waipende na
kuiheshimu.
“Rais
Magufuli utendaji wake ni wa kuigwa na viongozi wengi duniani kwani
anafanya maamuzi ya uhakika ikiwemo kukuza uchumi kwa kukusanya kodi na
kuziba mianya ya ubadhirifu wa mali ya umma,” alisema Profesa Bana.
“Pamoja
na kuwa Rais Magufuli amekuwa madarakani kwa kipindi kifupi, viashiria
vyote vinaonesha kuwa ni kiongozi imara na shupavu kutokana na mambo
makubwa ambayo ameyafanya kwa kipindi hiki kifupi. Katika kipindi hiki
kumekuwepo na nidhamu katika utumishi wa umma, kodi inakusanywa kwa
kiwango kikubwa na elimu ya msingi inatolewa bure kama Ilani ya Uchaguzi
ya Chama Tawala inavyosema,” alisema Profesa Bana.
Aidha,
Profesa Bana alisema kuwa wanaomlaumu Rais Magufuli ni wale ambao
hawajitambui na labda wanaona mianya ya ubadhirifu anayoendelea kuiziba,
wao wanakosa mapato, vinginevyo Rais anafanya vizuri katika kuliongoza
Taifa.
“Rais
Magufuli yuko sahihi kwa jinsi anavyosimamia vipaumbele vya serikali
ikiwemo elimu bure, kukusanya kodi na kuzuia mianya ya rushwa pia
dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda,” alifafanua
Profesa Bana.
Aliitofautisha
Serikali ya Awamu ya Tano na awamu nyingine zilizopita kwa kutokuwa na
kigugumizi katika kufanya maamuzi ikiwemo ya kuhamia Dodoma, kuondoa
wabadhirifu katika utumishi wa umma na kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima na fedha hizo kutumika kwa miradi ya maendeleo kama miundombinu,
afya na elimu.
Kwa
upande wake, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR
Mageuzi, Leticia Mosore amesema vyama vilivyoko katika Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), vimepoteza mwelekeo na vinashindwa kwenda na kasi
ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mosore
alisema ujio wa maandamano ya nchi nzima yaliyopewa jina la Ukuta, ndio
kifo cha Ukawa kwani kila chama kimekuwa kikihangaika kivyake.
Kuhusu
Ukawa kupoteza mwelekeo, alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk
Magufuli inayafanyia kazi kivitendo yale yote ambayo yalikuwa ni kero na
matatizo yaliyokuwa yakipigiwa kelele na upinzani, na hivyo ingewapasa
sasa kufurahia na kumpongeza kwa dhati kwa hatua hizo.
Alisema
Ukawa hivi sasa imekuwa ikitoa matamko ya ajabu, imekuwa kama umoja wa
kufanya vituko bungeni kila siku wanatoka na kususa, kufunga midomo,
mara wavae nguo nyeusi, na hata kuwatimua wale wanaotofautiana nao.
Katika
hatua nyingine, Mosore alisisitiza kwamba hatambui kusimamishwa
uanachama na uongozi katika chama hicho na ataendelea kufanya majukumu
yake kama kawaida kwa kuwa barua aliyopewa haijatoa sababu za hatua
hiyo. Alisema hakupewa haki ya kujitetea kwa mujibu wa Katiba ya chama
hicho ya mwaka 1992.
“Ninachoweza
kusema kwa ufupi, sitambui kusimamishwa uanachama kwa sababu sijaelezwa
sababu za kusimamishwa kwangu wala barua haielezi vifungu vya kikatiba
au kanuni zilizotumika kufikia maamuzi,” alisema Mosore.
Uongozi
wa wafanyabiashara ndogo maarufu kama ‘wamachinga’ wa soko la Mwenge
jijini Dar es Salaam, umesema hauungi mkono maandamano ya Ukuta kwa kuwa
maandamano hayo si halali kisheria. Uongozi huo, umesema maandamano
hayo hayana uhalali wa kisheria kwa kuwa tayari Jeshi la Polisi nchini
limeyazuia.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
Wafanyabiashara wa soko hilo, Omari Hamisi alisema hawapo tayari
kuumizwa na askari Polisi kwa sababu ya maandamano hayo ya Ukuta.
Alisema
wafanyabiashara hao wanamuunga mkono Rais John Magufuli kwa
kutojihusisha na maandamano hayo na badala yake wataendelea na kazi yao
ya kufanya biashara ikiwa ni njia ya kutekeleza kaulimbiu ya rais huyo
ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Kiongozi
huyo, alibainisha kuwa Dk Magufuli tangu aingie madarakani, amekuwa
akiwatetea wanyonge hasa wafanyabiashara ndogo hivyo kujihusisha na
maandamano hayo ni sawa na kumsaliti. Alisema rais huyo alionesha wazi
nia yake ya kutetea wanyonge alivyozungumza hivi karibuni na wananchi wa
Mwanza na baadaye Dar es Salaam ambako alielezea mikakati na mipango ya
Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwasaidia na kuwakomboa wanyonge.
“Dk
Magufuli ameonesha nia ya dhati kutetea wanyonge sasa leo hii
tukiandamana na kuunga mkono maandamano yaliyozuiwa na Polisi ni sawa na
kumsaliti,” alisema.
“Ukuta
ina maana gani na faida gani kwetu? Nchi yetu ni moja, taifa letu ni
moja, sisi ni wamoja hivyo hatukubali kufanya maandamano yasiyo na tija
kwetu na taifa pia,” alisisitiza na kueleza kuwa wafanyabiashara hao
wameshtuka na kuchoshwa na kitendo cha wanasiasa kuwatumia vijana
wachache kwa faida yao binafsi.
Maandamano
ya Ukuta yaliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
yakilenga kupinga kile wanachokiita udikteta wa Serikali ya Rais
Magufuli yanatarajiwa kufanyika kesho nchi nzima. Polisi na vyombo
vingine nchini vimetangaza kuwa maandamano hayo si halali.
Imeandika na Lucy Lyatuu, Halima Mlacha na Jonas Kamaleki, Maelezo.
|
Post a Comment