SHERIA
ya Fedha ya Mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada
ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu, imeanza
kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza kushuhudiwa
kutoka kampuni za simu.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya
Mawasiliano (TCRA), iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa
Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali
imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato, yaliyotolewa na kampuni za simu.
Taarifa
hiyo ilitolewa jana kwenye Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, imeonesha
Kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha
zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya
mabadiliko ya sheria, Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.
Mwakilishi
wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia
kamati hiyo kuwa kwa upande wa Kampuni ya Tigo, walikuwa wanatoa wastani
wa Sh milioni 250 kwa mwezi, lakini sasa wametoa Sh bilioni 1.48.
Barongo
ambaye ni Meneja Msaidizi, Kitengo cha Walipa Kodi Wakubwa TRA alikuwa
akizungumzia namna Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano na Udhibiti
wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS) unaosimamiwa na Mamlaka ya
Mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.
“Pamoja
na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu, kampuni za
simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye
kutoa, Baada ya hiyo, tuligundua kuwa sasa kamisheni nyingi zilipelekwa
kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye transfer zinapungua,”
alisema Barongo.
Aliendelea
kusema, “Kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo
tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia.” Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza
kuwa wabunge wanategemea Wizara ya Miundombinu kupitia sekta ya
mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.
Baada
ya Bunge kupitisha mabadiliko ya sheria ya fedha yaliyopitisha utozaji
kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za mkononi,
ulijitokeza mjadala ambao baadhi ya watu walidai ushuru huo utaathiri
wateja wa kampuni za simu na benki.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alifafanua kwamba serikali
imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au vyote kwa
kadri itakavyotozwa akisisitiza kwamba utalipwa na benki na kampuni na
si mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika.
Wakati
huo huo akielezea Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano na Udhibiti
wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS), Barongo alisema pia umesaidia kwa
kiwango kikubwa katika mapato kutoka kampuni za simu. Barongo alisema
kabla ya mwaka 2013, mtambo ulipokuwa haujapatikana, walishindwa kujua
kiwango cha kodi kutoka kwenye kampuni za simu.
Aliwaambia
wabunge kuwa awali kulikuwa na tatizo kubwa la kufahamu ni kwa kiwango
gani kampuni za simu zinazalisha ikizingatiwa kwamba, mfumo wa sasa wa
ulipaji kodi ni wa kujitathmini.
“Kwa
hiyo tunasema huu mfumo unasaidia, unaonesha sasa ni namna gani sasa
wanaweza (kampuni za simu) kutambua kuwa wanafuatiliwa kwa nyuma,”
alisema.
Awali,
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema mtambo huo wa TTMS
una kazi nyingi ikiwemo kutambua mawasiliano ya udanganyifu katika
mitandao na namba za ulaghai zinazotumika kwenye mawasiliano ya
kimataifa kinyume cha sheria.
Akizungumzia
hoja za baadhi ya wabunge waliotaka kufahamu ni kwa nini kampuni za
simu haziko kwenye walipa kodi wakubwa 10 wa mwanzo , Barongo alisema
hivi sasa zinapangwa kulingana na sekta. Hata hivyo alisema, itakapokuja
kwenye sekta ya mawasiliano, anaamini angalau kampuni tatu za simu
zitaonekana kwenye nafasi ya juu.
Aliisifu
kampuni mpya ya Halotel akisema inafanya vizuri. Kwa upande wa TTCL,
alisema bado haijatoa mchango wa kutosha katika mapato ya serikali,
jambo aliloshauri kuwa inahitaji kusaidiwa hatimaye iwe miongoni mwa
vyanzo vya mapato ya serikali.
|
Post a Comment