Wafanyikazi sita wa baraza la mji wa Ntugumo nchini Uganda wamesimamishwa kazi kwa madai ya kutovaa tai.
Kulingana na gazeti la Daily Nation, walisimamishwa kazi na afisa mkuu Kweyamba Ruhemba ambaye aliwapata na makosa ya sheria za baraza hilo kwa kuvaa mavazi kwa njia ambayo inatoa picha mbaya kwa wilaya hiyo.
Wote walipatikana bila ya tai.
Gazeti hilo limemnukuu Ruhemba akisema kuwa maafisa hao wamesimamishwa kazi kwa miezi miwili ili kuwafunza kuvaa kwa heshima.
Mapema 2017, wizara ya nguvu kazi ilitoa maelezo ikipiga marufuku nguo zinazoonesha ndani, zile za kubana kwa maafisa wasiovaa sare za kazi miongoni mwa wafanyikazi wa serikali.
Kulingana na gazeti hilo katibu wa wizara ya utumishi wa umma , bi Catherine Bitarakwate Musingwiire alisema kuwa maelezo hayo yanaenda sambamba na sheria za wizara ya utumishi wa umma.
Sheria ya utumishi wa umma nchini Uganda , ya mwaka 2010 inasema uwa maafisa watalazimika kuvaa kwa heshima kulingana na viwango vinavyokubalika katika jamii ya Uganda.
Gazeti la Daily Nationa linasena kuwa sheria hiyo hatahivyo imenyamaza kuhusu ni nini kitadhihirisha kwamba mtu amevaa kwa heshima ili kukubalika.
Katika sheria hiyo wafanyikazi wanawake wanahitajika kuvaa sketi ama rinda ambalo halipiti juu ya magoti na shati yenye heshima.
Marinda ama tisheti zinazoonyesha ndani , marinda ya kubana, sketi fupi, viatu vya chini na nywele zilizopakwa rangi vimepigwa marufuku .
Post a Comment