Ni hakika kabisa ili mtu afanikiwe kwenye ndoto yake aliyonayo ni
lazima awe na kiwango cha juu sana cha njaa au shauku (to be hungry) ya
kufikia ndoto yake; huwezi kufikia mafanikio makubwa sawa na unavyotaka
kama ndani yako hauna shauku ya kutosha ya kukufikisha kwenye mafanikio
hayo unayoyahitaji. Wenye njaa ya mafanikio ndio wanaoteka miliki na
nguvu za dunia; angalia wafanyabiashara wakubwa na wanasiasa wakubwa
duniani; hao wote na wengine wengi ukifatilia historia zao utakuta
pamoja na kupitia misukosuko mingi juu ya kufikia ndoto zao lakini
hawakukata tamaa ya kufuata na kuishi ndoto zao walizonazo. Ndani yao
njaa ya kufanikisha ndoto zao haikuzuiwa na kitu chochote kile mbele yao
bali walijitoa kwa dhati hadi kufikia hapo tunapowaona leo hii.
Nipo wazi kukuambia kuwa leo unahitaji njaa au shauku ya kutimiza
ndoto yako kwa kiwango cha juu sana kila siku ili uweze kuona matokeo
makubwa unayoyahitaji katikati ya maisha yako. Kumbuka watu wenye njaa
ya mafanikio na kutimiza ndoto zao huwa hawachoki mapema njiani ni watu
wenye hatua endelevu za kufuata ndoto zao (Unstoppable people); ni watu
wasiokoma kutengeneza picha mpya kila siku kwa ajili ya maisha yao ya
badae (Imagination people); hawachoki kutafutafuta wanachokitaka
(Uncommon people); ni watu wasiokata tamaa (refuse to give up); si watu
wenye kutoa sababu mbalimbali katika kuchukua hatua (no excuse is
acceptable to them); ni watu wenye kufanya vitu ambavyo wengi leo
hawavifanyi ili kesho wawe na maisha ambayo wengi watakuwa hawana.
Sababu 5 zifuatazo kwa nini unapoteza njaa au shauku ya kufanikisha ndoto yako:
1: Unapenda kuishi maisha ya watu wengine.
Kuna watu ni rahisi sana kuishi maisha ya watu wengine kuliko kuishi
maisha ya ndoto zao binafsi. Hii imekuwa ni sababu kubwa ya watu wengi
kuwapelekea kukata tamaa haraka pale wanapoona wamezidiwa viwango fulani
vya kimaisha na watu wanaowatizama. Kuwa na mtu unaweza kumtumia kama
mfano (role model) kwenye maisha yako si vibaya, ila ni mbaya sana pale
unapotaka kulingana na mtu huyo kwa muda mfupi huku haujui mtu huyo
amepitia magumu mangapi hadi akafikia hatua hiyo aliyopo leo. Unahitaji
kubadilika na kuishi maisha yako binafsi na si maisha ya mtu mwingine.
Acha kuiga maisha ya watu wengine na kuyaishi, kwani huko ni
kujishusha na kutokutambua uwezo mkubwa Mungu alioweka ndani yako. Kuna
watu wengi leo wameingia kuimba kwa ajili ya kuona watu fulani wanaimba
hatimaye wanapofikia mahali fulani na kuona wanapwaya katika kitu
walichokimbilia wanarudi nyuma na kukata tamaa, inakubidi utafute kusudi
na wito wa kwako duniani; usifanye mambo kwa kufuata watu wengine
wanavyofanya. Usiende kuimba kisa umemwona mtu fulani anaimba na
kukubalika, usiwe mwandishi kisa umeona kuna mtu mwandishi anafanya
uandishi na anakubalika; chunguza kipaji chako na amua kukitumia kwa
ufanisi ili ufikie viwango vya juu unavyovitaka binafsi.
2: Haujiamini na Unajilaumu binafsi kwa kila kitu.
Hofu na mashaka pamoja na kujilaumu binafsi juu ya kila kitu
unachofanya ni mojawapo ya tabia inayoweza kuwa sababu kubwa ya kupoteza
njaa na shauku ya ndoto yako. Unapofanya jambo fulani na kukosea au
usipolifanikisha kama ulivyokuwa unataka, huo si wakati mzuri kwako wa
kuanza kujilaumu na kupoteza imani juu ya uwezo wako ulionao, bali
unachotakiwa ni kujifunza kutokana na makosa hayo na kukubaliana na hali
hiyo ili uweze kuchukua hatua mpya zaidi itakayokuwezesha kuwa bora
zaidi kuliko mwanzo. Unapojilaumu binafsi kwa hatua ndogo na ya mwanzo
uliyoshindwa kufanikisha, unakuwa unaifunga akili yako isipate kuona
milango mingine ya kukusadia kutoka na kufanikisha jambo husika.
Chunga tabia ya kujilaumu bali kubaliana na matokeo madogo
uliyoyapata hata kama hayajakutosheleza sawa na ulivyokuwa ukitaka.
Kumbuka wewe unauwezo mkubwa sana ndani yako kuliko jinsi unavyofikiri,
unahitaji kufanikisha ndoto yako na si kukata tamaa mapema; jiamini na
amini unaweza zaidi sana ishi ndoto yako.
3: Unaridhika mapema sana.
Watu wengi sana wanapopata mafanikio kidogo tu kutokana na hatua
fulani wanazochukua katika malengo na mipango waliojiwekea, basi watu
hawa wanaridhika haraka na kusahau kabisa ndio kwanza pamekucha. Ndio.
hapo ndio kwanza pamekucha. Huwezi kuanzisha biashara leo baada ya kuona
wateja wamekuwa wengi basi ndio uridhike kwa kisa cha wateja kuwa wengi
kwako unaanza kudharau wateja wengine, tambua huko ni kukosa nidhamu na
kwa mtindo huo hautochukua muda mrefu utapoteza wateja wote na sifa
nzuri zote ulizokuwa nazo hapo mwanzoni.
Acha kuridhika mapema kwa unachokipata, tambua mafanikio hayana
mwisho ni jinsi wewe utakavyoamua kundelea kupigania ndoto yako ili
ufikie kipimo cha juu kabisa ambacho Mungu amekwisha kukupimia tangu
ukiwa tumboni mwa mama yako. Una uhalali wa kuwa na kiwango cha juu sana
cha mafanikio bila serikali yoyote duniani kukuingilia kama ni
mafanikio yaliyotokana na njia halali kabisa. Acha kuridhika mapema, na
kama ni hivyo basi Bill Gate na mabilionea wengine wote duniani
wasingefikia hapo walipo; acha kujipimia kiwango kidogo nje ya kile
Mungu alichokupimia tumboni mwa mama yako.
“Una
haki ya kutajirika ilimradi unafanya shughuli halali. Hakuna mwenye
haki ya kukupimia kiasi cha utajiri halali Mungu aliokupa.”
Reginald Mengi
4: Unapenda kufanyiwa kila kitu. Hautaki kuchukua hatua mwenyewe.
Angalia mara ngapi linapotokea suala la
kulichukulia hatua huwa unachukua hatua haraka mwenyewe pasipo kutaka
mtu mwingine akufanyie? Hilo ni swali kwako. Kuna watu kwenye maisha yao
ni kama vile hawana viungo vyote vya mwili; hawa ni watu wenye kupenda
kufanyiwa kila kitu na watu wengine hata vile ambavyo vilitakiwa
kufanyika na wao binafsi na vilivyo na umuhimu mkubwa kwao. Kumbuka
kuwa,“kufanyiwa kila kitu na mtu mwingine ni kuchagua kulaumu na kuumia kwa maumivu mengi.”
Punguza tabia ya kupenda kufanyiwa kila kitu
hata ambacho kipo kwenye uwezo wako wa kukifanya binafsi. Unapofanyiwa
kila kitu unaweza ukawa umechagua kufanyiwa vitu chini ya kiwango
ambacho ulikuwa unakihitaji; na hapo ndio mwanzo wa kutoa malaumu na
kusababisha kupoteza shauku ya kufanya upya jambo husika. Acha mara moja
tabia hii na amua mara moja kupenda kuchukua hatua mwenyewe ili uweze
kufikia mafanikio makubwa unayoyataka juu ya ndoto yako.
5: Umekata tamaa mapema.
Je, umekata tamaa mara ngapi kwenye kuifaata
ndoto yako? Usikubali kukata tamaa mapema hivi kwenye kuifata ndoto
yako ya maisha. Kukata tamaa mapema kwenye ndoto yako ni kuruhusu
kupoteza kila kitu ulichokianza na kuamua kuishi maisha yaliyo chini ya
kiwango chako. Usikubali kukata tamaa juu ya ndoto yako (Never giver up
on your dream).
Fanya zoezi hili:
1: Andika changamoto 5 unazoona zinakuzuia kuifata na kuishi ndoto yako sawa na unavyotaka.
2: Tumia changamoto hizo kama faida ya kukupa matokeo mapya na makubwa baada ya kuchukua hatua juu yake.
Post a Comment