Nilichojifunza katika maisha ni kwamba, kila mtu amebeba ndoto ya
kwake tena iliyotofauti na ya mtu mwingine, na zaidi sana kila ndoto ina
uzani na kiwango sawa na mwenye nayo alivyojiwekea.
Wapo wenye ndoto
kubwa zenye nafasi ya kupindua ulimwengu na kuleta matokeo makubwa
kwenye vizazi vingi duniani; Wapo wenye ndoto za kiwango (level) ya
kawaida wasiotaka kujisumbua sana katika maisha yao kutokana na hofu na
mashaka ya kuishia njiani.
Yote kwa yote kila mmoja anayo nafasi ya kushinda changamoto
anazokumbana nazo njiani kama ataamua, ili kuweza kufikia hatua ya mbali
ya kutimiza ndoto yake. Unayo nafasi ya kuamua uwe nganzi gani na
kubeba ukubwa wa ndoto gani katika maisha yako; hakuna mtu anayeweza
kukuzuia kama utamua kuwa na ndoto kubwa katika maisha yako, ilimradi
utambue nafasi gani unaipa ndoto yako ili iweze kutimia sawa na muda
ulionao na unaoishi hapa duniani.
Wapo watu walioandika historia kubwa katika ulimwengu na kuifanya
dunia iwashangae kutokana na nafasi walioitoa juu ya kuishi ndoto zao,
na hapo waliwafanya wengine waweze kuwa wajasiri wa kujaribu kufuata
ndoto za maisha yao baada yao. Hebu jiulize kama Thomas Edison angekata
tamaa kipindi hicho juu ya ndoto yake kwa kujaribu mara elfu moja
kutengeneza balbu ya umeme hadi akaweza; kama angekata tamaa mapema
njiani jiulize dunia ingepata wapi mchango wa ndoto yake hivi leo. Leo
hii tunatumia balbu za umeme kutokana na ndoto ya mtu aliyewahi kuishi
miaka iliyopita duniani, aliyejitoa kutimiza ndoto yake na kuacha
historia katika dunia. Jiulize wewe utaacha historia gani duniani? Je,
utakumbukwa kwa kutoa mchango juu ya jambo gani chini ya jua?
Nataka kukuambia unayo nafasi ya kuwa na ndoto kubwa katika maisha
yako inayoweza kupindua ulimwengu na kuifanya dunia ikukumbuke badae kwa
namna ambavyo umejitoa kikamilifu kusaidia wengine; unayo nafasi sasa
ya kutengeneza historia yako vizazi hadi vizazi kutokana na ndoto
utakayojiwekea na kuiishi katika maisha yako yote hapa duniani.
Wapo watu wengi wanaogopa kuwa na ndoto kubwa hii ni kutokana na sababu zifuatazo:
1: Hofu ya kushindwa kutimiza au kufanikiwa au kuishia njiani.
2: Hofu ya kukataliwa na wengine.
3: Hofu ya kukosa ujuzi au elimu kubwa.
4: Hofu ya kutokujiamini.
5: Hofu ya kuumia baada ya kushindwa.
6: Hofu ya hasara au kupoteza walichonacho.
Michael Jordan aliwahi kusema, “I’ve failed over and over and over
again in my life and that is why I succeed.” (Nimewahi kufeli na kufeli
na kufeli katika maisha na hiyo ni sababu iliyonifanya nikafanikiwa).
Kama Michael Jordan ambaye amekuja kuacha historia kubwa katika mchezo
wa basketi nchini marekani anakuambia mafanikio yake yametokana na
kujaribu na kushindwa mara nyingi; ni kwa nini wewe uwe na hofu ya
kushindwa kufikia ndoto yako. Ni kwa nini unaogopa changamoto zilizo
mbele yako katika kuitimiza ndoto yako? Amua leo hii kubadili mwelekeo
wa fikra zako na amini moja kwa moja ya kuwa unaweza kutimiza ndoto yako
haijalishi ni kubwa kiasi gani.
Napoleon Hill katika kitabu chake cha Think and Grow Rich anasema;
“Edison failed 1,000 times before he made the electric light. Do not be
discouraged if you fail a few times.” Les Brown anapenda kusema; “if you
do what is easy your life will be hard. but if you do what is hard your
life will be easy.” (Kama unapenda kufanya mambo marahisi tambua maisha
yako yatakuwa magumu. Ila kama unapenda kufanya mambo magumu maisha
yako yatakuwa marahisi). Huwezi kufanikiwa kwa kufanya mambo marahisi
marahisi yale yaliyokwisha patiwa majawabu (solution) na watu wengine.
Amua kuwa mbunifu kwa kufanya mambo magumu na mapya yatakayokupa
changamoto kuanzia ya kiakili na maisha, lakini mwisho wa siku yataleta
matokeo makubwa na chanya katika maisha yako.
Watu wanaokimbilia mambo marahisi siku zote huishia katika kiwango
(level) cha chini cha maisha; watu wa aina hii wamejawa na hofu
nilizotangulia kuzitaja hapo juu, na hii ndio sababu zaidi ya kuwafanya
watu wengi kubaki katika maisha ya umasikini na hali ya kati ya kiuchumi
katika maisha yao. Acha kuwa na ndoto ndogo ndogo ambazo hazina hata
thamani ya milioni ishirini unapozigeuza kwenye fedha. Hii ndio sababu
unabaki kwenye umasikini na maisha ya watu wa kiwango cha chini.
Kuwa
mwenye njaa ya kutimiza ndoto kubwa itakayokupa matokeo makubwa maishani
mwako.
Mwalimu Christopher Mwakasege amewahi kusema maneno haya katika
kuwafundisha vijana; “Kwa nini unasoma hata huelewi kwa nini unasoma
unataka upate cheti, halafu kikusaidie kufanya nini? Mwingine anatafuta
kozi ambazo ni nyepesi afaulu mitihani apate cheti. Nani alikuambia
Mungu alikuleta duniani ili uishi maisha mepesi. Kuna watu wengine
wameitiwa kutatua matatizo ya watu wengine; kuna watu wengine ambao
wameitiwa wawe watangulizi wapasue miamba kabla ya wengine hawajapita.
Na maisha yako hayawezi kuwa rahisi na maandalizi yako hayawezi kuwa
rahisi.”
Mwakasege anaendelea kusema; “Hawezi Mungu akakuweka na kukuandaa kwa
ajili ya kuwa kiongozi halafu utegemee kukaa kienyeji kienyeji saa hii,
haiwezekani. Waliopasua barabara ambazo tunazipita sasa hivi kwa lami
kwa dakika kidogo, waliangaika sana kupasua pasua mawe na kupasua pasua
miti na kuhakikisha kwamba imejengwa, iliwachukua muda mrefu kusogeza
hatua moja ya lami na kusogeza hatua moja ya barabara, sasa hivi wewe
unapita tu haraka; sikiliza! Maandalizi yenu yapo tofauti, wewe
unayeandaliwa kuendesha gari juu ya hiyo lami ni tofauti sana na
maandalizi ya yule aliyetengeneza hiyo lami. Hamuwezi kufanana.”
Ondoa jiwe la uoga na hofu ya kujiwekea maono na ndoto kubwa katika
maisha yako; hizo ni changamoto tu wala usiwe na hofu ya kuzitatua.
Kumbuka huwezi kukumbukana na changamoto kubwa kama ndoto yako ni
(level) ya chini au ya kawaida; bali kila mtu atakumbana na changamoto
zilizo sawa na kiwango cha ndoto yake aliyoibeba. Na kumbuka kadiri
unavyokutana na changamoto zenye kiwango cha juu na kuzishinda, ndio
unavyojiwekea mazingira mazuri ya kufikia ndoto yako uliyonayo. Kiwango
cha changamoto unazokutana nazo na kuzishinda ndio kinaamua nafasi yako
ya kesho utakayokuwa nayo.
Usikwepe changamoto yoyote katika maisha bali ikabili changamoto hiyo
kwa kujiamini na kwa moyo wa dhati ili ulete ushindi wa kiwango cha juu
zaidi katika maisha yako. Usilie na kujaribu kuzikimbia changamoto
zinazosimama mbele yako, bali furahi na zifaate ili kuzikabili na
kuzitatua. Na hapo ndipo utaona matokeo chanya na makubwa yakitokea
katika maisha yako ya kila siku. Ondoa jiwe la uoga, mashaka na hofu ya
kushindwa na kukataliwa mbele yako nawe utauona ushindi mkuu mbele yako.
Narudia tena; usiogope kuwa na ndoto kubwa kisa kukwepa changamoto
ambazo utakutana nazo. Usikwepe kufungua kampuni unayotaka kisa utakosa
fedha za kuiendesha; usiogope kuwa mwimbaji kisa kuna waimbaji wengi
wenye majina makubwa kuliko wewe; usiogope kutumia kipaji chako
ulichonacho kisa hauna ujuzi na elimu kubwa ya kufanya hivyo; usiogope
kuanza biashara au kujiajiri kisa hauna mtaji wa kuanzia au watu wa
kukusaidia (kuku-support) anza kidogo kidogo kwa ulichonacho utafika tu;
usiogope kufanya chochote kwa aina yoyote ile ya sababu inayojitokeza
mbele yako, amini unaweza na una uwezo mkubwa sana wa kufanya unachotaka
kama utaamua kufanya hivyo. Ondoa hilo jiwe la uoga lililo ndani yako,
lisukume nje pasipo uoga hadi uone ushindi wa mafanikio yako.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Post a Comment