0

Jukumu la Ulinzi na Usalama kwa ngazi ya chini lipo chini ya Serikali za Mitaa baada ya Serikali Kuu kuhamishia madaraka yake huko likiratibiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye kimsingi  kwa ngazi hiyo ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa husika.

Moja ya suala ambalo lilipata upotoshaji mkubwa kwenye mitandao ya kijamii ni kauli aliyotoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kutaka kuwatambua wakazi wa Dar es Salaam ambapo taarifa za kwenye mitandao ya kijamii zilizusha kwamba lengo lilikuwa ni kuwakamata watu wasio na kazi maalumu.

Kupitia Power Breakfast ya Clouds Fm Makonda amesema “Sikusema wasio na kazi maalumu wakamatwe kwa kuwa hatuna sehemu za kuwahifadhi hao wote watakaotiwa nguvuni, kimsingi huu ni upotoshwaji mkubwa uliofanyika kwenye mitandao ya kijamii, mimi nilitoa maelekezo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wawafahamu na kuwatambua watu wao na shughuli wanazozifanya”.

Makonda amesema jukumu la ulinzi na usalama kwa ngazi ya Mkoa lipo chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ambaye kimsingi ni Mkuu wa Mkoa na sio Meya wala mtu mwingine yeyote; ndiyo maana jukumu hilo ameamua kushirikiana na ngazi ya serikali ya mtaa kwani suala la ulinzi liliachiwa Jeshi la Polisi pekee na ndio maana lilionekana kulemewa.


“Hakuna mwenye uwezo wa kumzuia Mwenyekiti wangu wa Serikali ya Mtaa kwenda nyumba hadi nyumba akiwa na askari ili kuwatambua wakazi, suala la ulinzi ni jukumu letu sote … tukishindwa kuwatambua watu maana yake hata milioni 50 zitakazotolewa na Rais Magufuli ambapo Dar es Salaam itapata bilioni 28 na milioni 650 zitashindwa kuwafikia walengwa”. Alisema Makonda.

Kuhusu swala la ombaomba

Makonda amesema jumla ya ombaomba 687 walibainika kuwepo jijini Dar es Salaam huku asilimia 70 kati yao sio wakazi wa Dar es Salaam, na kusisitiza bado operesheni ya kuwaondoa inaendelea kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo hadi kufikia Agosti mwaka huu zoezi hilo litakamilika ili watoto ambao wanazurura wakiomba waweze kurejeshwa shuleni.

Post a Comment

 
Top