WATU wengi
hutegemea mifugo kwa riziki lakini hawafugi katika misingi inayotakiwa ili
kupata tija zaidi. Ufugaji wa wanyama humpa mkulima nyama na maziwa kwa
matumizi ya nyumbani na mapato kutokana na mauzo ya ziada.
Ama mifugo
pia ni chanzo cha samadi. Bidhaa zingine za wanyama zinazoweza kuuzwa ili
kupata pesa zinajumulisha ngozi, samadi ya kuongeza rutuba kwenye ardhi ya
kupanda mimea na pia kutoa kawi ya biogas, pembe, kwato na midomo ya ndege
ambavyo hutumika katika viwanda kuzalisha bidhaa zingine.
Zipo aina
mingi ya wanyama ambao mkulima anaweza kuwafuga kuanzia ng’ombe, mbuzi, kondoo,
ngamia, sungura, nguruwe na vile vile ndege wa nyumbani kama kuku, bata bukini,
bata mzinga, bata, hua (njiwa) na mbuni. Siku hizi pia wapo wakulima wanaofunga
kwale na kanga.
Chaguo la
mnyama wa kufuga hutegemea mambo mengi. Hata hivyo, wakulima wengi hufuga
wanyama ambao wana ujuzi wa kuwasimamia na wanawapatia mapato mazuri.
Katika
Makala haya tutajifunza namna ya ufugaji bora wa mbozi wa maziwa ambapo
tutaanza kuangalia jinsi ya kuanzisha mradi huo na mambo mengine ya awali.
Mbuzi
mara nyingi wanafahamika kama “ng’ombe wa maskini” kwa sababu nyingi. Kwa
yeyote anayetaka kufuga mbuzi kwa ajili ya maziwa, mbuzi anaweza kuwa rahisi
kumhudumia kuliko ng’ombe.
Gharama
za uanzishaji wa mradi wa mbuzi wa maziwa mmoja au hata watano ni ndogo
ukilinganisha na kuanzisha mradi wa ng’ombe wa maziwa. Chakula na zana za
kufanyia kazi pia ni za gharama nafuu. Kufuga ng’ombe wa maziwa kunaweza kuwa
changamoto kubwa kwa mtu anayeanza ufugaji, lakini kwa mbuzi ni sawa na
kutafuta mnyama mwingine rafiki zaidi ya mbwa.
Mbuzi wa
maziwa humpatia mkulima maziwa kwa ajili ya familia na kuuza ili kupata fedha.
Samadi ya mbuzi hutumika kurutubisha ardhi na mbuzi wenyewe wanaweza kuuzwa pia.
Kipato cha ziada kinachotokana na mazao ya mbuzi kinawawezesha wafugaji kumudu
gharama za matumizi zikiwemo kulipa gharama za nyumbani kama chakula na huduma
nyingine; kulipia gharama za shule kwa watoto wao ama kuwekeza katika miradi
mingine kama kilimo na biashara zingine.
Kwa miaka ya
karibuni serikali imekuwa ikihimiza ukulima endelevu ambao unahusisha ufugaji
wa kisasa wenye tija kwa kuangalia mifugo ambayo siyo tu itakuwa fahari ya
mkulima, bali inaweza kumpatia manufaa kibiashara.
Taasisi
mbalimbali zimekuwa zikijitokeza kuwasaidia wakulima kwa mafunzo na kuanzisha
miradi ya ufugaji wa mbuzi wa maziwa na ingawa siyo wakulima wengi waliopata
mafunzo hayo ama kuanzisha miradi hiyo, lakini kwa wale wachache ambao
wameanzisha miradi ya mbuzi wa maziwa, wameona faida zake.
Linapokuja
suala la kufuga mbuzi wa maziwa, wengi wanapata hofu na kujiuliza maswali mengi
kwamba wanahitaji ardhi yenye ukubwa gani ili kuwafuga, watawalisha nini, na
namna gani ya kuwahudumia.
Lakini MaendeleoVijiji ni mtandao ambao uko
kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima na wafugaji, pamoja na wananchi wengine
wanaotaka kuanzisha miradi ya aina hiyo, na ujasiriamali mwingine na tutakwenda
hatua kwa hatua ili kila mmoja aweze kuelewa.
Ufugaji wa
mbuzi wa maziwa unaweza kufanywa mahali popote, iwe mjini ama kijijini, kwa
sababu mbuzi hawa, tofauti na mbuzi wa kienyeji wanaofugwa zaidi kwa ajili ya
nyama, wanaweza kufugwa kwa njia ya ‘Zero Grazing’, kwamba wanaweza kufungiwa
kwenye banda maalum na kulishwa.
Kanuni
za ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa
Mbuzi wa maziwa
wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu
na kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na
ng’ombe.
Kutokana na
umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia wanaweza kuhudumiwa na
familia yenye nguvukazi na kipato kidogo. Uzao wa muda mfupi unamwezesha
mfugaji kupata mbuzi wengi kwa kipindi kifupi.
Wanyama hao
hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, na mazao mengine kwa matumizi ya
familia na kuongeza kipato.
Hata hivyo, ufugaji
bora wa mbuzi wa maziwa lazima uzingatie kanuni zifuatazo:-
1) Wafugwe
kwenye banda au zizi bora
2) Wachaguliwe
kutokana na sifa za koo/aina na lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au vyote kwa
pamoja)
3) Wapatiwe
lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili
4) Kuzingatia
mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na wataam wa mifugo
5) Kuweka na
kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji
6) Kuzalisha
nyama au maziwa yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko
Ziko faida
nyingi za ufugaji wa mbuzi wa maziwa na miongoni mwazo ni:
Lishe bora
Maziwa ya
mbuzi ni mazuri kwa afya na yana ladha nzuri mno kuliko ya ng’ombe! Pia maziwa
hayo yana protini nyingi kuliko maziwa ya ng’ombe. Ni mazuri kwa lishe, rahisi
kunywewa na yana viinilishe vingi kwa sababu yana madini mengi ya kalsiumu,
fosforasi na klorine kuliko maziwa ya ng’ombe.
Kwa kuwa
makala haya hayajalenga kueleza umuhimu wa madini hayo katika mwili wa
binadamu, hatutaweza kujadili bali tutajadili katika makala nyingine, hata
hivyo, ieleweke kwamba, maziwa ya mbuzi yana uwezo mkubwa wa kuongeza kinga
katika mwili (immune) kwa watoto na hata watu wazima. Wapo watu hawawezi kunywa
maziwa ya ng’ombe kwa sababu wana mzio (allergy), lakini hakuna anayeweza
kushindwa kunywa maziwa ya mbuzi.
Kama unafuga
ng’ombe wa maziwa na mbuzi wa maziwa, nakushauri maziwa ya mbuzi uyatumie
nyumbani halafu ya ng’ombe ndiyo uyauze. Lakini kama unao mbuzi wengi ama
wanazalisha maziwa ya ziada, bado unaweza kuyauza ambapo bei yake ni zaidi ya
mara mbili kwa ile ya maziwa ya ng’ombe.
Nyama ya
mbuzi ni tamu sana na inaliwa na watu wengi. Lakini mbali ya maziwa na nyama,
wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa wana faida kubwa ya kutengeneza mtindi pamoja
na siagi, mazao ambayo yana soko kubwa. Kimsingi, maziwa ya mbuzi yana mafuta
mengi hivyo ni rahisi kupata siagi nyingi zaidi.
Kiuchumi
Mbuzi wana
gharama ndogo sana ya chakula kulinganisha na ng’ombe. Ng’ombe mmoja anaweza
kula chakula kinachowatosha mbuzi watatu mpaka sita kwa siku, kutegemeana na
aina (breed) na mahitaji ya mbuzi husika. Mbuzi wanaweza kula nyasi, magamba ya
miti na kadhalika, vyakula vingine ambavyo ng’ombe hawezi kula. Mbuzi wanazaa
mara mbili kwa mwaka wakati ng’ombe anazaa mara moja. Ukipata bahati ya mbuzi
wanaozaa mapacha, unaweza kuongeza mifugo ndani ya muda mfupi. Kwa kawaida,
mbuzi hubeba mimba kwa muda wa wiki 20 au miezi mitano (siku 150) na
hunyonyesha kwa miezi miwili. Kumbuka pia mbuzi pia ni wastaarabu kuliko
ng’ombe.
Ukiwa
mfugaji wa maziwa huna haja ya kuhofia kuhusu uchakataji wa maziwa yako ili
utoe siagi, jibini na samli, kwa sababu soko la uhakika la maziwa lipo, tena
kubwa hapa Tanzania.
Nchini
Kenya, kwa mfano, wakati lita moja ya maziwa ya ng’ombe inauzwa kwa KShs. 40
(takriban Shs. 800 ya Tanzania), maziwa ya mbuzi yanauzwa katika KShs. 80 na
100 (TShs. 1,600 na 2,000) kwa lita.
Kuhusu kiasi
cha maziwa unayopata kila siku, mbuzi hawako nyuma sana ya ng’ombe. Wakati
ambapo ng’ombe aliyetunzwa vizuri anaweza kutoa mpaka lita 15 au 20 kwa siku,
mbuzi wa maziwa wa uzao bora anaweza kutoa mpaka lita 7 kwa siku na katika nchi
ambayo mbuzi wa kienyeji wanaweza kutoa lita 2 kwa siku, hii ni faida kubwa
kuwa na mbuzi wa maziwa.
Kwa maana
nyingine, kuwa na mbuzi watatu ni sawa na kuwa na ng’ombe mmoja, jambo ambalo
ni la faida pia, kwa sababu ikitokea ugonjwa ng’ombe huyo mmoja anaweza kufa,
lakini mbuzi watatu hawawezi kufa wote, unaweza kuwaokoa wengine, hivyo
kuendelea kuwa na maziwa.
Kwa upande
mwingine, mbuzi wanahitaji usimamizi mdogo kuliko ng’ombe.
Mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu ufugaji wa mbuzi
wa maziwa
Kama
nilivyokwishaeleza hapo juu, maziwa ya mbuzi ni mazuri na yana madini muhimu
kwenye mwili hivyo basi kila mmoja anapaswa kujifunza kuyatumia.
Maziwa ni
chakula muhimu chenye madini muhimu mwilini na pia ndiyo njia mojawapo ambayo
watu huambukizwa magonjwa haswa kwa kupuuza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa.
Lakini
lazima ifahamike kwamba, ufugaji wa mbuzi wa maziwa ni uwekezaji mzuri hasa kwa
wakulima wenye mashamba madogo na hata yule mkazi wa mjini ambaye anaweza
kulitumia eneo lake la uwani kufuga.
Ifahamike
pia kwamba, ukulima ni sawa na biashara na biashara nzuri lazima iwe na
mpangilio mzuri hasa kwa matumizi ya pesa zinazoapatikana. Kabla ya kuanzisha
mradi wa ufugaji wa mbuzi wa maziwa, lazima uwe na mpango mzuri hata kama
unaanza na mbuzi wawili, kwani kwa kufanya hivyo utaweza kujua gharama zake na
hiyo itakusaidia pia hata kuongeza mbuzi wengine na kupanua mradi.
Mpango wako
wa mradi ndio pia utatoa taswira ya matumizi ya fedha kwa sababu kama hutakuwa
na matumizi mazuri ya pesa hizo huenda iwe vigumu kununua vitu muhimu ili
kuendeleza biashara hiyo.
Kwa maana
hivyo, hata baada ya kuanzisha mradi huo, ni vyema ukumbuke kuweka rekodi ili
kujua ikiwa unapata faida au hasara na ili kuweza kubaini matatizo yanayoikumba
biashara yako.
Ufugaji wa
mbuzi wa maziwa ni mradi unaoweza kuanzishwa katika vikundi, lakini pia unaweza
kuanzishwa na mtu mmmoja mmoja.
Wakulima hao
ni lazima waunde vikundi au vyama ambavyo watafaidika navyo na pia vitasaidia kupigania
kupata bei nzuri ya bidhaa zao pamoja uimarishaji wa sera za serikali ili
kuwawezesha kufanya biashara yao chini ya usaidizi mzuri kutoka kwa serikali.
Tanzania ni
mojawapo ya nchi zilizo na maofisa kilimo na mifugo (maofisa ugani) waliohitimu
vizuri lakini wananchi wengi huwa hawawatumii maofisa hawa ipasavo ambao kazi
yao kuu ni kukuhudumia. Ukitaka kufuga vizuri utafanikiwa ikiwa utatafuta msaada
na ushauri kutoka kwa maofisa hao wa serikali walio kwenye eneo lako.
Maswali ya
msingi yanayoulizwa na watu wengi:
Mbuzi anatoa maziwa kiasi gani?
Kwa
wastani, mbuzi anaweza kutoa lita 800 kwa mwaka. Hata hivyo, kiasi hiki
hutofautiana kutegemeana na aina ya mbuzi, lakini hii inamaanisha kwamba,
anaweza kutoa lita kuanzia lita 2 hadi 7 kwa siku. Hii inategemea aina ya
mbuzi, namna ya utunzaji na chakula unachomlisha. Kwa matumizi ya nyumbani tu,
kiasi hicho ni kikubwa kwa siku.
Kumbuka
kwamba, mbuzi anakamuliwa kwa kipindi cha miezi 10 kwa mwaka na wanaachwa kwa
miezi miwili ili kuwapa nafasi ya kuzaa tena. Mbuzi hutoa maziwa mengi baada ya
kuzaa (kitaalam wanasema ‘kidding’). Ukiwa na mbuzi mmoja au wawili, huwezi
kukosa maziwa kwa mwaka mzima.
Ladha ya maziwa ya mbuzi ikoje? Ni matamu kuliko ya
ng’ombe?
Kama
nilivyoeleza hapo awali, maziwa ya mbuzi yana ladha nzuri ingawa katika
mazingira mengi, ni wachache ambao wanaweza kutofautisha. Maziwa ya mbuzi ni
meupe sana.
Mbuzi
pia wanatofautiana kutokana na aina, ambapo mbuzi aina ya Nubian maziwa yao yana mafuta mengi kuliko mbuzi aina ya Saanen kama ilivyo kwa ng’ombe aina ya Jerseys
na Holsteins. Lakini kuna mambo mengine yanayochangia maziwa kuwa na mafuta
mengi au kutokuwa na mafuta, kama uachishaji wa unyonyeshaji na ulishaji.
Inagharimu kiasi gani kufuga mbuzi wa maziwa?
Hii
inatofautiana kila mwaka na kila mahali, kutegemeana na mazingira ya
upatikanaji wa chakula, na aina ya chakula unachomlisha mbuzi huyo. Katika
mazingira ya kijijini ambako unaweza kumfungulia mbuzi akajichungia mwenyewe,
gharama ni ndogo sana, pengine ni dawa za chanjo. Mbuzi anahitaji chakula
kuanzia nusu tani hadi tani mbili kwa mwaka, kutegemeana na aina ya mbuzi,
kiwango cha ubora wa chakula chenyewe, na mazingira mengine kwa ujumla.
Mbuzi
pia anahitaji chakula cha nyongeza kama mahindi au mchanganyiko wa mahindi na
ngano, pumba za nafaka na nafaka nyinginezo. Kwa kawaida, inategemea na nini
kinacholimwa kwenye eneo husika au kinachopatikana. Mbuzi jike anahitaji
chakula cha ziada ili kutoa maziwa mengi.
Upatikanaji
wa vyakula hivyo ndio utakaoonyesha ni gharama kiasi gani unazotumia kumlisha
mbuzi huyo. Suala la gharama za tiba nalo ni muhimu.
Gharama
nyingine za kuangalia ni zile za kuanzia kama banda la mbuzi, uzio, vifaa vya
kulishia na kunyweshea, uhifadhi wa nyasi, na vifaa vya kukamulia.
Angalia,
usitumie gharama kubwa, bali unaweza kuanza na vile vinavyopatikana katika
mazingira uliyopo. Usiwaze kujenga banda la gharama wakati unaweza kutumia miti
ya kawaida tu. Usinunue chakula kama nyasi zinapatikana kwa wingi.
Sina nafasi ya kutosha, je, bado naweza kufuga mbuzi
kadhaa?
Mbuzi
ni wanyama wanaofaa kufugwa katika eneo dogo nyumbani. Mbuzi wanahitaji eneo
lenye ukubwa wa futi 12 x 20 kwa kila mmoja kama unatumia mfumo wa Zero
Grazing, na katika mazingira ambayo mbuzi wanakwenda kuchunga wenyewe,
wanahitaji eneo dogo. Banda linapaswa kuwa kavu kwa sababu mbuzi siyo kama
ng’ombe, hawawezi kulala kwenye tope.
Mbuzi wanaweza kuwa wanyama rafiki?
Ndiyo.
Ni wanyama welevu na wenye kujenga urafiki. Kama kuna mbuzi mkorofi, basi ujue
hakutunzwa vizuri ama alikuwa akinyanyaswa. Lakini kumbuka kwamba mbuzi ni
mifugo, siyo kama mbwa. Hupaswi kuwafunga Kamba muda wote, bali wanapokwenda
kuchunga hasa kama katika mazingira uliyopo wanaweza kuharibu mali zilizopo kwa
kuwa wanapenda kucheza na huvutiwa na vitu vingine. Jihadhari, usiegeshe gari lako
jirani na banda la mbuzi, kwa sababu wanaweza kuliharibu kwani wanaweza kupanda
juu n ahata kuvunja vioo.
Vipi kuhusu maradhi?
Mbuzi
mara nyingi ni wastahimilivu wa mazingira na magonjwa na wana matatizo machache ikiwa watatunzwa vizuri. Kwa kawaida wana
wadudu tumboni, hasa minyoo (na hawawezi kuishi bila kuwa nao), lakini mtaalam
wa mifugo anaweza kusaidia kuwatibu minyoo hiyo kwa kuanzisha program ya
kuondoa minyoo.
Ugonjwa wa Mastitis
(kuvimba kwa kiwele) mara nyingi huwakumba mbuzi wengi, lakini huo unaweza
kudhibitiwa katika suala la ukamuaji.
Kwa
ujumla, kama unataka kufuga kibiashara au una mbuzi wengi ndipo utamhitaji
ofisa ugani wa mifugo, lakini kama unao wachache, ni rahisi kuwamiliki na
kukabiliana na changamoto ndogo ndogo.
Vipi kuhusu majukumu?
Mbuzi
wanatakiwa kulishwa na kunyweshwa maji kila siku. Kama wanakamuliwa, unapaswa kuwakamua kila baada ya saa 12
– lakini hiyo haimaanishi kila mshale unapogonga, na inaweza kuwa saa 1 asubuhi
na saa 1 usiku au mchana na usiku mnene.
Unatakiwa
kusafisha vizimba vyao na kuweka matandazo mahali wanapolala.
Mbuzi wanatakiwa kupunguzwa pembe zao mapema kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwemo kuogopa wasije
wakaumizana wanapocheza ama kupigana. Pia wanatakiwa kupunguzwa kwato kila
mara, kwa sababu kwao za mbuzi wanaofugwa bandani tu hukua haraka kuliko za
mbuzi wazururaji. Punguza kwato mara moja kwa mwezi.
Nimeambiwa nyama ya mbuzi ni tamu sana, je ni kweli?
Nyama
ya mbuzi (chevon au cabrito kwa Kiingereza) inafanana kidogo
na nyama ya kondoo. Watu wengi wanaipenda kwa sababu ni tamu, lakini kwa sababu
mbuzi jike anatakiwa azae ilia toe maziwa, wengi wanategemea kwamba atazaa dume
ambaye baada ya muda ataliwa.
Ninapaswa kuwa na beberu ninapoanza ufugaji?
Hapana,
hususan kama ni mfugaji mdogo wa mbuzi. Inaweza kuongeza gharama za uchumi
bure. Ukishajifunza kuhusu aina za mbuzi, nasaba haiwezi kuwa na umuhimu sana,
kwa sababu unaweza kuamua kutumia mabeberu kadhaa tofauti. Unaweza kukodisha
bebeeru au unaweza kutumia mabwana mifugo kupandikiza mbuzi wako.
Kuna jambo la ziada ninalopaswa kujua?
Ndiyo!
Uamuzi wa kununua mbuzi haupaswi
kufanywa kwa ghafla bila uhakika. Mbuzi atachukua muda wako na kiasi cha
fedha. Atarejesha faida ikiwa utamtunza vyema. Kuna mambo mengi ya kujifunza.
Hata wataalam na wazoefu wa kufuga nao hujifunza kila siku. Mbali ya hayo,
huhitaji kuwa mtaalam ndipo uanze ufugaji wa mbuzi wa maziwa. Kwa ujumla,
hakuna njia ya uhakika ya kupata elimu na uzoefu bila mwenyewe kuanza ufugaji.
Ni wajibu wako wewe kuingia kwenye ujasiriamali huo.
Post a Comment