UMOJA wa Nchi za Ulaya (EU) umesema
jitihada zimeanza kuonekana za Serikali ya Awamu ya Tano katika
kuhakikisha lengo namba saba la Mpango wa Malengo ya Maendeleo Endelevu
(SDGs) linatekelezwa nchini.
Lengo
hilo limezungumzia suala la upatikanaji kirahisi, kwa bei nafuu na kwa
uhakika wa nishati. Hayo yalibainishwa na Balozi wa Umoja wa Ulaya wa
Tanzania na Afrika Mashariki, Roeland Van de Geer wakati wa uzinduzi wa
kitabu cha ‘Empowering Tanzania: Energy for Growth and Sustainable
Development kinachozungumzia namna ya kuiwezesha Tanzania kuboresha
upatikanaji wa nishati kwa maendeleo ya nchi hiyo.
Van de Geer alisema upatikanaji wa
nishati ya uhakika kwa Tanzania ndio ufunguo mkubwa wa maendeleo hasa
katika maeneo ya vijijini. “Kitabu hiki kimelenga kutoa maelezo ya jumla
kuhusu namna EU itasaidia sekta ya nishati nchini.
Kinazungumzia hatua zilizochukuliwa
zamani na zitakazochukuliwa siku zijazo kwa lengo la kuhakikisha lengo
namba saba la SDGs linafikiwa,” alifafanua Geer. Alisema umoja huo
umekuwa ukitoa misaada katika kuboresha upatikanaji wa nishati kwenye
maeneo ya vijijini kupitia miradi midogo ya maji iliyopo katika maeneo
ya kusini mwa Tanzania na miradi ya nishati ya jua katika visiwa vya
Ziwa Victoria.
Aidha, alisema pia EU imekuwa ikisaidia
kuimarisha miradi ya miundombinu ya kusafirisha na kusambaza nishati
kwa ajili ya kufikia vijiji kupitia gridi na nje ya Gridi ya Taifa. “Pia
umoja huu ni mshirika wa Tanzania katika kufanikisha mageuzi ya msingi
ya sekta ya nishati kwa kuongeza ufanisi na uwezekano wa upatikanaji wa
fedha,” alisema.
Post a Comment