0

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani humo kuwaondoa wakuu wa shule za sekondari wasioendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.

Aidha, amepiga marufuku madawati kutumika katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo mikutano ya hadhara na kwamba madawati mengi huharibika haraka na kusababisha wanafunzi kushindwa kuyatumia.

Alisema hayo jana wakati wa ziara ya kukagua usambazaji wa madawati unaoendelea katika halmashauri hiyo na kujionea usimamizi mbovu wa wakuu wa shule unaosababisha wanafunzi kupata matokeo mabaya katika mitihani ya kitaifa.

Mtaka alisema wanafunzi wengi hawapewi mitihani ya majaribio mara kwa mara na matokeo yake walimu wamekuwa wakisubiri mitihani ya kufunga shule na ya kitaifa hali ambayo inawafanya kupata matokeo mabaya.

“Kumekuwepo na utaratibu wa viongozi wa vijiji kutumia madawati katika mikutano ya hadhara na kuanzia sasa madawati ni marufuku kuhama katika darasa husika kwa lengo la kwenda kufanyia mikutano ya wananchi na hicho ndio chanjo cha uharibifu wa madawati,” alisema Mtaka.

Awali, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Rosemary Kirigini alisema halmashauri hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 29,000 na mpaka sasa madawati 19,800 yamesambazwa katika shule.

Alisema halmashauri inaendelea kutengeneza madawati kupitia Chuo cha Ufundi cha Binza na kwa sasa kina uwezo wa kutengeneza madawati 1,000 kwa wiki ambayo yatapelekwa katika shule mbalimbali wilayani humo.

“Tumeendelea kutengeneza madawati kwa wingi kupitia chuo chetu cha ufundi na kwa sasa tuna uwezo wa kutengeneza madawati 1,000 kwa wiki na wilaya ilikuwa ina upungufu wa madawati 29,000 na kwa sasa tayari tumeshatengeneza madawati 19,000 ambayo tayari tumesambaza,” alisema.

Post a Comment

 
Top