SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
imekiri kuwepo kwa matukio yanayotishia amani na utulivu Pemba ikiwemo
kuibuka kwa migomo katika vyombo vya usafiri na hujuma zinafanyika
katika mashamba ya wananchi.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, wakati akijibu swali la
Mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni Pemba, Sheha Hamad Matar, aliyetaka
kufahamu serikali inachukua hatua gani katika kupambana na matukio ya
hujuma Pemba ambayo yanawaathiri zaidi wafuasi wa CCM.
Aboud alisema matukio yote hayo
yanakusanywa na serikali kupitia vyombo vya ulinzi kwa ajili ya ushahidi
ambao utapelekwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa hatua
zaidi za kisheria.
Hata hivyo, alisema juhudi za viongozi
wakuu wa serikali zimechukuliwa kwa ajili ya kukagua waathirika wa
matukio ya vitendo vya hujuma kisiwani Pemba na kwamba na uchunguzi
unaendelea kukomesha matukio hayo.
“Mheshimiwa naibu spika nataka
kuwaambia wajumbe na wananchi kwa ujumla kwamba matukio yote yanayotokea
Pemba viongozi wetu wanayafahamu na tayari wamefanya ziara kutoa pole
kwa waathirika……lakini tunawaambia wananchi kwamba wahusika
watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Aboud.
Alisema inasikitisha kuona wananchi wa
Pemba wanafanya matukio ya ajabu wakati asilimia 99 ni waumini wa dini
ya Kiislamu na kwa sasa wapo katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
Post a Comment