Serikali ya Nigeria
imetangaza mpango wa kutoa ajira kwa vijana zaidi ya nusu milioni ambao
wamemaliza chuo kikuu lakini hawana ajira, hatua hii ni mojawapo ya
jitihada za serikali za kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa
vijana.
Mpango huo ni sehemu ya uwekezaji katika jamii ulioahidiwa
na rais Muhammadu Buhari wakati wa kampeni yake ya kugombea urais.
Taarifa ya Naziru Mikailu kutoka Abuja inasimuliwa na Halima
Nyanza.Mpango huo unaoitwa N-Power Teach ni wa kwanza wa aina yake
katika taifa kubwa barani Afrika.Ni mmoja kati ya mikakati mitatu ambayo serikali imesema itatoa ajira za moja kwa moja kwa watu laki tano. Watafanya kazi ya ualimu katika shule za msingi na sekondari nchi nzima.
Wale ambao maombi yao ya kazi yatapita, wataajiriwa kwa muda wa miaka miwili na kulipwa kiasi cha dola mia moja na kumi na tano kwa mwezi.Vile vile watapewa komputa na vifaa vyake kamili ili ziwasaidie katika kutekeleza majukumu yao.
Mikakati mengine miwili ni N-Power Knowledge ambao utatoa mafunzo kwa wanigeria elfu ishirini na tano katika masuala ya teknolojia, na N-Power Build, ambao unatarajiwa kutoa mafunzo kwa wananchi wengine wapatao elfu sabini na tano katika maeneo ya huduma za ujenzi, mapishi, pamoja na ufundi wa magari na masuala ya gesi.
Serikali imesema imetoa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo katika bajeti yake ya mwaka huu.
Hata hivyo, serikali zilizopita zilikuwa na mipango mikubwa ambayo haikufaulu utekelezaji wake.
Hivyo, wengi wanataka kuona jinsi gani rais Buhari atafanikiwa katika utekelezaji wake wakati ambapo mapato ya nchi yamepungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Licha ya kuwa na rasilimali nyingi, nchi nyingi za Afrika zinaishi katika hali duni kutokana na vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali.
Post a Comment