0


Mwenyekiti wa kijiji cha Lubasanze wilaya ya Morogoro amenusurika kupigwa na wananchi wake kwa kile kilichodaiwa kutosoma matumizi na mapato tangu achaguliwe ikiwa ni pamoja na kutuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kuwaruhusu kuingiza mifugo ambayo imekuwa ikiharibu mazao ya wakulima wa kijiji hicho.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara wa kijiji hicho uliohudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya Morogoro Salum Jazza,wananchi hao wamefikia uamuzi huo wakidai kuchoshwa na Mwenyekiti huyo ambaye amekuwa  akizorotesha maendeleo ya kijiji hicho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Sevelini Vunde amekiri kupokea fedha kutoka kwa wafugaji ambazo amedai alizitumia kwa matumizi halali huku diwani wa kata ya Kolelo akikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Mwenyekiti huyo ili awaruhusu wafugaji kuingia kijijini hapo.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Morogoro Salum Jazza amesema chama hicho hakitawavumilia viongozi wanaotokana na Chama cha Mapinduzi pamoja na watumishi wa umma ambao watasababisha kudhoofisha maendeleo katika maeneo yote ya wilaya ya hiyo.

Post a Comment

 
Top