Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.
SHIRIKA la
Utangazaji la Taifa (TBC) limefanya upembuzi yakinifu wa kufunga mitambo
ya FM yenye uwezo wa Kilowati moja katika eneo la Mbambabay Wilayani
Nyasa Ili kuongeza usikivu wa Redio za TBC.
Kauli hiyo
imetolewa leo Bungeni Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Nape Nnauye wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbinga
Vijijini, Mhe. Martin Msuha aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa
kuongeza uwezo wa kurusha matangazo ya Kituo cha TBC Songea ili wananchi
wa tarafa hizo wapate habari kupitia TBC.
Mhe. Nape ameeleza kuwa Matangazo ya Redio ya Taifa kupitia mtambo wa masafa ya kati yaani ‘’Medium Wave’’
wenye nguvu ya Kilowati 100 yalikuwa yakisikika vizuri katika Wilaya
mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma wakati mtambo huo ulipokuwa ukifanya kazi.
‘’Tangu mwezi
Julai, 2013 mtambo huo haufanyi kazi kutokana na uchakavu na hivyo
kuathiri usikivu wa matangazo ya TBC katika maeneo kadhaa”, alisema Mhe.
Nape.
Alisema kwamba,
kwa kutambua umuhimu wa Wananchi katika kupata matangazzo, TBC
ililazimika kuhamisha mitambo yake miwili ya Redio yenye uwezo wa
Kilowati moja kwa kila moja iliyokuwa imefungwa eneo la Mshangano,
Songea na kuifunga eneo la juu la mlima wa Matogoro-Songea ili usikivu
Wake usambae katika eneo kubwa zaidi.
‘’Baada ya kufunga mitambo hiyo, matangazo ya TBC Songea yameboreshwa”, aliongeza Mhe. Nape.
Ameongeza kuwa
katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/17 Wizara yake imetenga fedha za
maendeleo kwa ajili ya kufunga mtambo eneo la Mbambabay.
‘’Kazi hiyo ya
uboreshaji wa matangazo katika eneo Hilo itaanza mara tu fedha za
kununua na kufunga mitambo hiyo zitakapotolewa”, alisema Mhe. Nape.
Aidha, alisema
kwamba kutokana na uwezo mdogo wa mitambo ya FM inayotumika kwa sasa,
mawimbi yake ya sauti hayafiki mbali sana ukilinganisha na yale ya
mitambo ya ‘’Medium Wave’’ iliyokuwa ikitumika awali ambayo yanafika eneo kubwa zaidi la Mkoa wa Ruvuma zikiwemo Tarafa za Hagati, Mbuji na Mkumbi.
‘’Kukabiliana
na changamoto za usikivu hafifu katika maeneo kadhaa Mkoani Ruvuma, TBC
imeshafanya upembuzi yakinifu wa kufunga mitambo ya FM yenye uwezo wa
Kilowati moja katika eneo la Mbambabay Wilayani Nyasa Ili kuongeza
usikivu wa Redio za TBC,”alisema Mhe. Nape.
Post a Comment