Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto inasikitishwa na
inalaani vikali tukio la kuuawa kwa kuchinjwa, mwanamke Oliver Erasto
(23) na mtoto wake Emmanuel (3), wakazi wa eneo la Zinga, kata ya Dunda,
wilayani Bagamoyo, kutokana na wivu wa kimapenzi.
Wizara
inakemea maauji hayo, yanayodaiwa kutekelezwa na Frowin Mbwale mkazi wa
Kawe, Dar es salaam, ambaye ni mme wa marehemu, kwani yamesababisha
kukatisha maisha ya mama na mtoto, katika kipindi ambacho Taifa
linahimiza uzingatiaji wa mchango na haki za wanawake katika maendeleo
ya taifa, na mwitikio wa haki ya kuishi ya Mtoto katika mipango na
programu za maendeleo endelevu.
Wizara
inasisitiza kutambua kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa wanafamilia
liko mikononi mwa kila mwananchi, hivyo jamii inawajibu wa kusaidia
udhibiti wa ukatili na mauaji katika familia na jamii zetu. Jamii ikiwa
na uelewa wa pamoja katika haki za wanawake na watoto katika jamii,
itawezesha kuwekeza katika haki ya kuishi ya Mtoto, na kuendelea
kuwaamini wanawake kwamba wanaweza kutoa mchango mkubwa wa kuendeleza
familia zao, na taifa likaweza kupiga hatua kufikia maendeleo endelevu.
Wizara
inapenda kupongeza Polisi mkoa wa Pwani na wananchi walitoa taarifa za
kuwakamata watuhumiwa wa mauaji haya, na tunaamini kuwa watakapofikishwa
mbele ya vyombo vya sheria haki itaweza kutendeka.
Wizara
inapenda kutoa pole kwa familia za marehemu hao waliopoteza maisha kwa
kuchinjwa na kuawa, na kuwaombea kuwa na moyo wa subira katika kipindi
hiki cha majonzi makubwa. Wizara inaitaka jamii itambue kuwa hakuna
mwenye haki ya kukatisha uhai wa mtu mwingine, na mwanamke na mtoto
anahaki ya kuthaminiwa utu wake, bila ubaguzi wowote ambao unaweza
kukatisha maisha yao.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
Post a Comment