RAIS
John Magufuli leo atafanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi baada ya
kukaa nchini siku zote tangu ashike madaraka ya kuiongoza Tanzania
Novemba 5, mwaka jana kwa kuzuru Rwanda.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Kikanda na
Kimataifa, Rais Magufuli atatoka kwa mara ya kwanza nje ya anga ya
Tanzania baada ya siku 151 kwa mwaliko wa Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Taarifa
hiyo ilisema Dk Magufuli atakuwa na ziara ya siku mbili ya kikazi
katika nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na
ambayo pia ni mshirika wa karibu wa Tanzania.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, wakati wa ziara hiyo, Rais Magufuli na mwenyeji
wake Rais Kagame wanatarajiwa kuzindua Daraja la Kimataifa la Rusumo
pamoja na Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) ambacho ni kituo muhimu
chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kituo
hicho katika mpaka wa Tanzania na Rwanda, siyo tu muhimu katika
kurahisisha mwingiliano kati ya nchi hizo mbili, lakini pia kitaboresha
uhusiano na matumizi ya Rwanda katika Bandari ya Dar es Salaam.
Baada
ya sherehe za uzinduzi, viongozi hao wawili watakwenda mjini Kigali
ambako watafanya mazungumzo kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili na
pamoja wataweka shada la maua kwenye Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari
mjini Kigali ikiwa ni kukumbuka mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka
1994.
Ikiwa
ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu achaguliwe Oktoba 25, mwaka
jana, ziara hiyo ni kielelezo cha jinsi Tanzania inavyoimarisha uhusiano
wake na majirani zake.
Akiwa
Mwenyekiti wa EAC, ziara hii ya kwanza nje ya nchi ya Rais Magufuli
akiifanya katika ukanda huo, pia inaonesha msimamo wake wa kisiasa
katika kuimarisha mchakato wa utengamano na mahusiano kati ya nchi
wanachama wa EAC.
Katika
hatua nyingine, vyombo vya habari vya Rwanda mbali na kueleza kuwa
Tanzania ni mshirika mkubwa wa nchi yao kiuchumi, ikiwa inatumia Bandari
ya Dar es Salaam kusafirisha na kupokea shehena ya asilimia 60, pia
wananchi wake ni watu wanaoshirikiana kijamii.
Vilieleza
kuwa mbali ya wananchi hao wa Rwanda, baadhi yao kuishi Tanzania,
lakini wanaiona kuwa ni kama makazi yao ya pili. Aidha, vilisema kuwa
Rais Kagame ameeleza kuvutiwa kwake na Rais Magufuli hasa msimamo wake
katika kukabiliana na rushwa.
|
Post a Comment