0


Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu nchini Tanzania-SUMATRA, imeanza kuendesha zoezi la ukaguzi na ukamataji wa daladala zinazokiuka leseni ya usafirishaji.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Mamlaka hiyo Bw. David Mziray, katika kipindi cha siku tatu zilizopita mamlaka hiyo imeendesha zoezi ambapo jumla ya daladala 105 zimekamatwa na wahusika wake kuwekwa nguvuni.

Bw. Mziray amesema daladala hizo zimekamatwa kwa makosa mbalimbali mojawapo ikiwa ni kukatiza njia, kuongeza nauli kiholela pamoja na lugha chafu na kwamba zoezi hilo la ukaguzi limekuwa likifanywa kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Mziray amefafanua kuwa kati ya daladala hizo, 36 tayari wahusika wake wameshafikishwa mahakamani katika mahakama ya wilaya ya Kinondoni na kwamba hatua ya kuwafikisha huko inatokana na kusitisha kwa muda utaratibu wa faini baada ya wamiliki wa vyombo vya usafiri kufungua kesi kupinga utaratibu wa faini.

Ameongeza kuwa wao kama wasimamizi wa sekta ya usafirishaji nchini wamelazimika kufikia hatua hiyo baada ya huduma ya usafiri jijini Dar es salaam kuonekana kama haina usimamizi kutokana na kwamba walipewa dhamana ya kuviendesha vyombo hivyo kujifanyia mambo kiholela hasa nyakati za jioni ambapo mahitaji ya usafiri yamekuwa makubwa.

Post a Comment

 
Top