Simba mmoja
aliyetoroka mbuga ya taifa ya wanyamapori ya Nairobi nchini Kenya
amepigwa risasi na kuuawa na maafisa wa kutunza wanyamapori baada ya
kumshambulia na kumjeruhi mtu mmoja.
Simba huyo alikuwa ameingia maeneo ya makazi karibu na kituo cha kibiashara cha Isinya.Msemaji wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) Paul Gathitu ameambia kituo cha redio cha Capital FM kwamba maafisa walilazimika kumpiga risasi mnyama huyo kwa sababu alikuwa anatishia usalama wa watu.
Alisema maafisa hao walikuwa wametumwa wakiwa na nia ya kumdhibiti lakini akawa mkali zaidi.
Kisa hicho kimetokea siku chache tu baada ya simba mwingine kutoka mbugani na kumjeruhi mzee wa umri wa miaka 63 katika eneo la Cabanas, karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta.
Mwezi uliopita, simba wengine wanne walitoka mbugani na kuingia eneo la makazi Lang’ata.
Post a Comment