RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli (picha ya Maktaba)
Hatimaye serikali imetengua kitendawili cha
lini ahadi ya Rais John Magufuli ya kutoa Sh. milioni 50 za maendeleo kwa kila
kijiji nchini itatekelezwa, kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu
mwaka jana.
Aidha, katika mpango wa utekelezaji wa ahadi hiyo, serikali
imetenga Sh. bilioni 811 na imeshaanza kushirikisha wadau mbalimbali ili kupata
maoni ya kuendesha mchakato huo kwa ufanisi na tija.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya
kikao cha wadau waliokuwa wakijadili rasimu ya mpango huo mwishoni mwa wiki,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa,
alisema serikali itaanza kutoa fedha hizo kuanzia mwaka ujao wa fedha.
"Kwa kuanzia, fedha hizo zitatolewa kwa awamu tatu
katika kipindi cha miaka mitano,” alisema na kuongeza:
"Fedha hizo zitatolewa benki kabla ya kutolewa kwa vikundi
mbalimbali kama Vicoba na Saccos kulingana na taratibu zitakazowekwa."
Kwa mujibu wa mpango huo, mchakato utaanza na mikoa 10 nchini
iliyo nyuma katika kutumia huduma za kifedha. Mikoa hiyo, kwa mujibu wa taarifa
ya utafiti ya Finscope ya mwaka 2013 ni Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya,
Shinyanga, Geita, Kagera, Dodoma, Rukwa na Ruvuma.
Akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema mkutano
huo ulilenga kupata maoni ya wataalamu namna bora ya kutekeleza mpango huo.
Akizungumza kwa niaba ya waziri, Kaimu Mkurugenzi, Maendeleo ya
Sekta Binafsi, Uwekezaji na Uwezeshaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Victor
Mwainyekule, alisema mawazo yaliyopatikana yatazingatiwa ili kuboresha kazi
hiyo, yenye lengo la kupambana na umasikini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Wanawake (TWB),
Zablon Yebete, alisema mpango huo ni uwekezaji mkubwa kwa Watanzania unaopaswa
kuungwa mkono na vyombo vya fedha na wadau wengine nchini.
Kwa mujibu wa mpango huo, walengwa watapatiwa mafunzo ya
ujasiriamali kabla ya kupatiwa fedha.
Post a Comment