Halmashauri
ya wilaya ya Mvomero inaanza kusafisha na kuweka mipaka ya barabara na
mitaro kwa kila upande, kutenganisha maeneo ya ufugaji na yale ya
mashamba katika vijiji vinavyozunguka bonde la Mgongolwa ili kukabiliana
na migogoro na vurugu za mara kwa mara zinazojitokeza ambazo
husababisha vifo vya watu na wanyama, uharibifu wa mali na majeruhi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero, George Mkindo,
amesema hayo wakati wa mkutano wa hadhara ulioitishwa na waziri wa
kilimo, mifugo na uvuvi, Mwigulu Nchemba, ukishirikisha vijiji
vinavyozunguka na kulitumia bonde hilo ambapo amesema mipaka hiyo
inatarajiwa kuanza kuwekwa mapema wiki hii na mkandarasi kutoka kiwanda
cha Sukari cha Mtibwa kwa kusafisha barabara yenye urefu wa kilometa 11
ikiwa na upana wa mita saba kwa kila upande kuzunguka eneo la mgogoro,
na katikati yake utachimbwa mtaro ili mifugo isivuke upande wa malisho
kwenda mashambani, huku mkuu wa wilaya ya Mvomero Betty Mkwasa akisema
wameweka mipango ya muda mrefu na mfupi kukabiliana na migogoro.
Mbunge wa Mvomero Suleiman Sadiq amesema zoezi hilo litashirikisha
na kuzingatia wataalam wa halmashauri wakiwemo wa ardhi, viongozi wa
vijiji na kwamba kikosi kazi kutoka wizara ya ardhi nao wamefika
wilayani humo kuanza upimaji na uwekaji mipaka, na kushauri jeshi la
polisi kuimarisha ulinzi ili shughuli za maandalizi ya kilimo ziendelee
huku akimuomba rais Dk John Magufuli kufuta hati miliki zidi ya mashamba
pori waliyopendekeza, baada ya kufanikiwa kuyafutia umiliki mashamba
saba kati ya 33 yaliyopendekezwa.
Waziri Nchemba aliyetaka jeshi la polisi kufanya doria za mara kwa
mara katika maeneo hayo badala ya kusubiri tatizo kuwa kubwa, amewaeleza
wananchi hao kuwa mipaka peke yake haitatosha kuondoa migogoro baina ya
pande hizo mbili kama kila mmoja hataheshimu matumizi yake na
kuzingatia utawala wa sheria, na kwa kila mmoja kutambua thamani ya
shughuli anayofanya mwenzake huku akiwaonya kuacha kuishi kwa visasi,
chuki na udanganyifu wa matukio.
Post a Comment