John Nkoroma(kushoto) na Sudi Mtutuma
(kulia) wazazi wa watoto. Hapa wakiwa kando ya kisima kinachodaiwa kusababisha
vifo vya watoto hao vilivyotokea Februari 9, 2016 wilayani Liwale-Lindi (Picha: Mwandae Mchungulike)
Na Mwandae Mchungulike-Liwale Lindi
Watoto
wawili wamefariki dunia baada ya kudumbukia kwenye kisima cha maji kilichopo
jirani na makazi yao.
Tukio
hilo la kusikitisha limetokea februari 9 majira ya saa kumi jioni katika kijiji
cha Mtakuja kata ya Nangando
wilaya ya Liwale mkoani Lindi ambapo watoto hao walizama na kufa maji
walipokuwa wakicheza na wenzao kando ya kisima hicho.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa polisi wilayani hapa, Bw. Raphael Mwandu amesema kuwa watoto hao
walifikwa na umauti huo walipokuwa wakicheza na wenzao jirani na kisima hicho
kinachomilikiwa na Bw. Mohamed Nguwate (44) ambae ni mtendaji wa kijiji cha
Mtawatawa kata ya Kiangara wilayani Liwale.
Aidha,
Mwandu aliwataja marehemu hao kuwa ni
Pili Nkoroma (3) Mwanafunzi wa shule ya awali Montessori na Asnat
Sudi Mtutuma (2) wote wakazi wa Kijiji cha Mtakuja.
Akiongea
na mwandishi, Asha Makumba ambae ni shuhuda wa tukio hilo amesema kuwa siku hiyo
alikuwa akielekea nyumbani kwa mama yake ndipo alipofika eneo la tukio na kuwakuta
watoto wakilia na kupiga mayowe huku wakitaja majina ya marehemu hao na kusema
kuwa wamezama kisimani.
“Binafsi
nilishtushwa na kupata uoga lakini gafla nikapata ujasili na kuamua kuwaopoa
watoto hao waliokuwa wakielea juu ya kisima” alisema Asha.
Asha
aliongeza kuwa baada ya kuwatoa watoto hao ambao walionekana kulegea na matumbo
yao kuwa makubwa kuliko kawaida, aliamua kupiga yowe zaidi ili apate msaada na ndipo
majirani pamoja na wazazi wa watoto hao walipokuja eneo la tukio na kujaribu
kuwapatia huduma ya kwanza bila mafanikio.
Nae
Mwahamisi Ng’oloko (Mama wa marehemu Pili) anasema baada ya kuona mwanae yupo
katika hali hiyo alichanganyikiwa lakini baadhi ya watu waliokuwepo eneo la
tukio walimtuliza na kumshauri ampigia simu mume wake aitwae John Emeli Nkoroma
“Mume
wangu alifika baada ya dakika chache kwakuwa hakuwa mbali na eneo la tukio na
akaamua kuwachukua watoto wote wawili akishirikiana na majirani waliokuwepo na
kuwakimbiza hospitali ya Wilaya Liwale lakini baada ya daktari kuwapima alisema
kuwa watoto hao walikuwa tayari wameshafariki dunia” Alisema Mwanahamisi kwa
uchungu mkubwa huku akitokwa na machozi.
Baadhi
ya mashuhuda wa tukio hilo wamemtupia lawama mmiliki wa kisima hicho Bw. Nguwate
kuwa amekiacha kisima hicho wazi bila kukifunika hali ambayo inahatarisha
usalama wa watoto na wapiti njia hasa kipindi hiki cha mvua.
“Tumekuwa
tukimpigia kelele sana Bw. Nguwate juu ya kukiziba kisima hicho bila mafanikio
na zaidi amekuwa akijibu kuwa tuwachunge
watoto wetu” Alisema Sudi Mtutuma baba wa marehemu Asnat.
Kwa upande wake Bi. Subira Likunja,
ambae nae alishuhudia tukio hilo amesema kuwa siku ya tukio wangeweza kupoteza
watoto zaidi ya wawili kwani katika eneo hilo kulikuwa na watoto wane waliokuwa
wakicheza ambao ni Nafati Chipandu na Ramadhani Mbwigage. Wengine ni Asnati na Pili (Ambao ni marehemu)
Kwa upande wa kamanda wa polisi wa Wilaya Bw. Raphael Mwandu, nae ametoa rai kwa wananchi
wote wa Liwale kuwa makini hasa kipindi hiki cha mvua na kuwataka watu wote
ambao wamechimba visima kuvifunika haraka ili kuepusha ajali na pia magonjwa ya
milipuko kama kipindupindu.
Post a Comment