WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wazidi kuiombea Serikali
kwani kazi ya kutumbua majipu ina mitihani mikubwa. “Tulikuwa hatufikii
lengo kutokana na kuwa na wafanyakazi serikalini ambao walikuwa
wanatorosha mali za serikali, lakini hao ndio tunakufa nao,” alisema
Majaliwa na kuongeza kuwa serikali imekuwa ikifuata sheria na utaratibu
pasipo kumuonea yeyote wakati wa utumbuaji majipu hayo.
Waziri
Mkuu alisema hayo jana mjini hapa wakati akiwa mgeni rasmi kwenye
sherehe za kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist Assemblies Of
God Tanzania (EAGT), Dk Abel Mwakipesile. Askofu Mwakipesile anakuwa
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo baada wa Askofu wa kwanza Moses Kulola
kufariki Agosti 29, 2013.
Pia
Waziri Mkuu alizungumzia suala la kuboresha elimu ya msingi na
sekondari na kubainisha kuwa kuanzia Julai serikali itaongeza fedha kwa
ajili ya mpango wa elimu bure. Majaliwa alisema ni muhimu kuiombea
Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa ikisimamia uwajibikaji kwani
utumbuaji majipu unahitaji maombi zaidi kutokana na kuwa na mitihani
mingi.
“Wengi
hawapendi kuguswa maslahi yao, mtuombee kazi ya kutumbua majipu ni
ngumu,” alisema na kuongeza kuwa serikali itafanya kazi kwa kufuata
sheria na taratibu na haitamuonea mtu.
Alisema
ni takribani siku 100 sasa tangu Rais John Magufuli awe madarakani,
lakini amefanya mambo mengi na anatakiwa kuungwa zaidi mkono. “Serikali
inaanza kupitia maeneo yote muhimu yatakayofanya Watanzania kupata
huduma kwa ukamilifu na moja ya maeneo yatakayoangaliwa katika bajeti
ijayo ni kupunguzwa kwa vifaa vya gharama ya ujenzi,” alisema.
Pia
alisema zipo baadhi ya taasisi za dini zinazotumia vibaya nafasi za
kuingiza bidhaa bila ushuru na kuwanyima fursa wale wenye malengo
mazuri. “Tunafuatilia taasisi zinazotumia mgongo wa dini kupitisha vitu
visivyo halali,” alieleza.
Aidha,
alisema atakuwa na kikao na viongozi wa dini zote maaskofu, mashehe na
wachungaji ili kujadili mambo gani yanayotakiwa kufanywa kati yao na
serikali ili kuwa kitu kimoja. Aliwaasa watumishi wa serikali kufuata
kanuni na sheria katika kuhudumia wananchi wenye matatizo mbalimbali.
“Mwananchi
apokelewe, asikilizwe na ahudumiwe na kama huduma haipo kwake aelekezwe
kwa kuipata, na kama kuna mtumishi anaona hawezi hayo atupishe, kwani
tunataka kuona Watanzania wanapata huduma iliyo bora,” alibainisha
Waziri Mkuu.
Alisema
kama kuna mtumishi ambaye anaona haendani na kasi ya utendaji kazi ya
Serikali ya Awamu ya Tano apishe kwani kuna wasomi wengi wanaohitaji
ajira. Pia alisema kuendelea kutoa huduma nzuri lazima mapato ya
serikali yanayokusanywa yasimamiwe na kukusanywa kwa ufasaha.
Waziri
Mkuu alisema anajua kuna kundi litakasirika kutokana na utendaji kazi
wao, na kuongeza, “wanaosema hii ni nguvu ya soda wanajidanganya, hii
sio nguvu ya soda. Najua kuna kundi litakasirika kwani tumedhamiria na
jitihada zetu ni kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinarudi kwa
ajili ya kusaidia wananchi.
“Bajeti
ijayo ya serikali fedha nyingi zaidi zitapelekwa kwenye maboresho ya
elimu nchini na kuanzia Julai tutaingiza kwenye bajeti ili suala hilo
liwe endelevu,” alisema akizungumzia mpango wa elimu bure.
Aliwataka
Watanzania kuwa wavumilivu kwani mkakati wa serikali katika kuboresha
elimu ni mzuri, lakini umeanza na changamoto nyingi, lakini wataendelea
kuboresha kutokana na serikali kuwa na mpango mzuri kwenye jambo hilo.
Pia alisema ubora wa elimu utaendelea kuimarishwa.
Kwa
upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist Assemblies Of God
Tanzania (EAGT), Dk Mwakipesile alisema kanisa hilo lina malengo ya aina
mbili ambayo ni ya kiroho na kimwili. Alisema kwa sasa kanisa hilo lina
jumla ya makanisa 5,000 Tanzania nzima huku wakiwa na majimbo zaidi ya
90 na Kanda tisa.
Alisema
pia kanisa hilo lina miradi mbalimbali ya kijamii pamoja na kiuchumi.
‘’Watanzania wana matumaini na serikali katika kuboresha huduma za jamii
hivyo harakati za kutumbua majipu zinawapa matumaini kuwa fedha
zitaenda kuboresha huduma za jamii,” alisema Askofu Mkuu Dk Mwakipesile.
Naye
Katibu wa EAGT, Leonard Mwizarubi alisema kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’
inaleta hamasa kubwa kwa kanisa, kwani wanaamini uchumi utaimarika.
“Endeleeni kuchukua hatua mbalimbali za kuleta unafuu wa maisha tupo
nyuma yako Hapa ni Kazi Tu,’’ alieleza.
|
Post a Comment