![]() | |
|
SERIKALI
imesema itaendelea kuhakikisha wanafunzi wanaosoma nje wanakuwa katika
mazingira salama, na tayari watu watano waliohusika na tukio la
kushambuliwa kwa wanafunzi wanne wanaosoma India wanashikiliwa.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Ramadhan Mwinyi aliyasema hayo
jana Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi wa tukio lililotokea
Bangalore India.
“Tulipata
taarifa kuwa wananchi wetu ambao ni wanafunzi wa Bangalore India
walishambuliwa baada ya raia wa Sudan kumgonga raia wa India kwa gari na
kisha kufariki dunia, ambapo kuanzia hapo palitokea mtafaruku wa
kushambulia watu wenye asili ya Afrika waliokuwepo maeneo hayo,”
alieleza Balozi Mwinyi.
Alisema
baada ya tukio hilo wanafunzi hao wa Kitanzania wakitokea chuo
walisimama maeneo hayo ili kujionea ni nini kimetokea lakini wao pia
walichanganywa na kuanza kushambuliwa na raia hao wa India kwa kuwa
walikuwa hawatofautishi watu, bali walikuwa wakishambulia raia wote
wenye asili ya Kiafrika.
“Katika
tukio hilo raia wetu wanne walishambuliwa vibaya na baadaye walipelekwa
hospitali na kupatiwa matibabu. Kufuatia hilo balozi wetu nchini humo
amefuatilia hili na ameandika barua ya kibalozi kutaka Serikali ya India
kueleza ni kitu gani kimetokea na kueleza jinsi gani wanawalinda raia
wetu,” alieleza.
Aidha,
alisema jana Balozi wa Tanzania nchini humo amefanya ziara ya kutembelea
jimbo hilo na atazungumza na raia ili kuhakikisha usalama wao
unalindwa.
Pia
alisema jana alimuita Balozi wa India nchini na kufanya naye mazungumzo
na alimhakikisha kwamba tayari hatua zimeshachukuliwa na tamko
limeshatolewa la kilichotokea Bangalore na wameahidi kwamba
watahakikisha wahusika wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Alisema
katika hatua za awali tayari watu watano wameshakamatwa na ulinzi wa
wanafunzi umeimarishwa na kuahidi wataimarisha usalama zaidi ili
wananchi walio nje waishi kwa usalama na mabaya zaidi yasijitokeze.
Aidha,
Balozi Mwinyi alisema kuna tukio lingine limetokea juzi jioni la
mwanafunzi Mtanzania Christian Benjamin Mutandisi aliyekuwa akisoma Chuo
cha Koshys ambaye alipata ajali ya pikipiki na kufariki dunia papo hapo
na kubainisha kwamba baada ya uchunguzi wamegundua kwamba ajali hiyo
haihusiani na tukio la Bangalore.
“Tumegundua
kwamba mwanafunzi huyo hakuvaa kofia ngumu, tumepata taarifa kwamba
Jumuiya ya Watanzania inaendelea na taratibu za mazishi. Hivyo tukio
hili halihusiani kabisa na lile la Bangalore,” alisema.
Pia
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa, Dk Augustine Mahiga alilitolea taarifa tukio hilo jana
bungeni mjini Dodoma kutokana na Mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 47
uliotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).
Zitto
alisema pamoja na kauli hiyo, Serikali ya India iombe radhi kwa Serikali
ya Tanzania kwa kushindwa kuwalinda wanafunzi hao wanaosoma nchini mwao
kwa kufuata taratibu na sheria.

Post a Comment