Ni vigumu
kuelezea moja kwa moja kujiamini maana yake nini? Lakini mtazamo wa mwanadamu
juu ya namna wenzake wanavyomchukulia inaweza kuwa kutafsiri ya neno kujiamini.
Ikiwa utajilinganisha na wengine na hatimaye kuhisi aibu, ujue unakabiliwa na
tatizo la kujiamini.
kuna mambo
mengi yanayoweza kumfanya mtu asijiamini mbele ya wenzake, kiasi cha kujiona
duni kwa hili na lile na wakati mwingine hali hiyo humfanya ashindwe kufanya
hata mambo ambayo anayajua na kwamba amekuwa akiyafanya kila siku, Kisaikolojia
huu ni ugonjwa ambao unaweza kuathiri uwezo wa mtu , namaanisha kwamba mtu
anaweza kuwa si mlemavu wa miguu, lakini akatembea mbele za watu upande upande,
anaweza kuwa na akili lakini akajikuta hawezi kuzitumia kwa sababu si mwenye
kujiamini.
Kama ilivyo
kwa magonjwa mengine, kuponywa kwa tiba, tatizo hili la kutokujiamini nalo
linatakiwa litibiwe. Zipo njia nyingi ambazo mtu anaweza kuzitumia kujenga hali
ya kujiamini, yako mambo muhimu ya msingi ambayo mtu akiyazingatia na
kuyafanyia kazi anaweza kuondokana na hali ya kutokujiamini.

kujizoeza kujiamini
Njia moja
muhimu sana kisaikolojia ya kujenga hali ya kujiamini ni kupenda kusikiliza
maneno ya kutia moyo na yenye ujasiri kutoka kwa watu maarufu. Kwa mfano, viongozi
wenye msimamo, watetezi wa haki za binadamu, wanasiasa wanaotetea maslahi ya
nchi bila hofu na kadhalika. Hotuba na maneno yao yakipata sehemu kubwa katika
akili ya mtu, lazima yatajenga hali ya kujiamini kama wale anaowasikiliza.
kubali matokeo
Ifahamike
kuwa ukiwaza kwa kina sana juu ya mahitaji yako, zao litakalofuata hapo ni
akili kukuletea sababu za kushindwa kufanikisha mambo unayoyataka. Sababu hizo
ukizipa nguvu sana ya kuziwaza zitakupa jibu la haiwezekani. Unapokuwa na
mawazo yenye mlango huo wa kutokufanikiwa, uwezo wako wa kujiamini hushuka na
kujikuta unashindwa katika mambo uyafanyayo. Katika maisha lazima mtu akawa na
wakati wa kuachia mawazo yake na kukubaliana na matokeo yaliyopo hasa pale hali
ya kushindwa inapokuwa kubwa.
Pata Msaada toka kwa watu wengine
jambo
jingine la muhimu katika kuhitimisha uwezo wa mtu kujiamini ni kupata msaada wa
mawazo kutoka wa watu wengine ambao ni makini katika maisha yao. Kama kuna
jambo ambalo linakuwa gumu katika mawazo yako na limekosa ufumbuzi kiasi cha
kukufanya usijiamini, washirikishe wengine wakusaidie na kukutia moyo wa
kuendelea kukabiliana na hali yako ya kutojiamini.
Pendelea kukaa mbele
Katika
kujenga hali ya kujiamini ni vizuri zaidi unapokuwa shule, ofisini, kwenye
mikutano, semina ukawa na tabia ya kuketi nafasi za mbele. Ni ukweli kuwa, watu
wengi hawapendi kukaa sehemu za mbele kwa sababu ya hofu ya kuonekana kwa
urahisi na pengine kuwa wa kwanza kuulizwa au kuchangia hoja, tabia hiyo
huondoa hali ya mtu kujiamini. Ili kujenga ujasiri ni vema mtu akapendelea
kuketi vitu vya mbele na mara nyingi kuwa wa kwanza katika kufanya mambo.
Mwonekano sahihi
Namna mtu
mwenyewe anavyouweka mwili wake linaweza kuwa ni tatizo la kumfanya ashindwe
kujiamini. Kwa mfano,mtu kama si mlemavu lakini akajikuta anatembea miguu
upande, mabega juu, kichwa chini au juu sana au kutembea akiwa anadundika kama
mpira, ni vibaya kwa vile kitaalamu huchangia kumuondolea mtu ujasiri mbele za
watu.
Ushauri
wangu ni kwamba mtu anatakiwa kuupa mwili wake umuhimu na kuuweka kama
alivyoumbwa, haifai kuwa mtu wa kuinama na kuficha uso, kusimama tenga pale
unapoitwa au kuwa mbele za watu. Si vema pia kujipapasa mwilini au kutazama
pembeni. Ni vizuri kila mtu kulinda mwonekano wake wa asili mbele za wenzake.
Kutembea haraka
Njia rahisi
ambayo imethibitika kuweza kumuondolea mtu hali ya kutokujiamini ni kutembea
kwa mwendo wa haraka. Haipendezi unapokuwa njiani kutembea kama mgonjwa,
uliyechoka. Ukiwa hivyo ni rahisi sana kuwafanya watu wakukodolee macho ambayo
yatakufanya wewe uhisi tofauti. Utembeaji wa haraka una faida nyingi, lakini
kubwa kabisa ni kuwafanya watu wengine wakuone wewe ni mtu wa kazi usiyetaka
kupoteza muda wako, mtu makini na mwenye mipango. Kitaalamu mwendo unaoruhusiwa
ni wa asilimia 25, usizidi sana kiasi cha kuonekana kama unakimbia.
pingana na wengine
Mtu akijiona
duni mwenyewe ni rahisi kwake kudhani kuwa watu wengine ndiyo wenye mambo ya
kweli na hivyo kujikuta akifuata mkumbo na kupotoshwa katika ukweli. Ili mtu
aweze kuwa sahihi katika mawazo ya vile anavyoamini ni lazima awe na tabia ya
kupingana na wenzake. Ni jambo baya kukubaliana na watu katika mawazo yao bila
kupinga katika kile unachoamini, kufanya hivyo kunaweza kuyafanya maneno ya
uongo ya wengine yakaaminika na kuuacha ukweli wa mtu asiyejiamini ukipuuzwa
kwa sababu tu hakuwa na ujasiri wa kukabiliana na hoja za wenzake.

Post a Comment