Hili ndilo kaburi la shaaban Robert lililopo Vibambani Machui mjini Tanga.
Shaaban Robert alizaliwa
tarehe 1 Januari, 1909 katika kijiji cha Vibambani kata ya Machui mjini Tanga.
Jina lake linawakilisha taaluma ya fasihi na
lugha ya Kiswahili katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Asili ya jina Robert ni mwajiri wa babu
yake ambae aliitwa 'Roberto' asili yake kutoka Italy. Bibi yake Shaaban
alipokuwa na ujauzito alikuwa akianika uduvi katika ufukwe wa bahari ya
hindi mjini Dar es Salaam, eneo la kurasini katika shamba la minazi.
Wakati uchungu ulipomjia alijifungua hukohuko ufukweni kwa msaada wa
wanakijiji.
kutokana na kuzaliwa ufukweni babu yake
Shaaban alipewa jina la Ufukwe. Lakini babu yake Shaaban alipokwenda
kazini na kumpa taarifa mwajiri wake mzungu juu ya kupata mtoto wa
kiume, mzungu yule kwa furaha na namna alivyoshibana na babu yake
Shaaban alitaka mtoto yule apewe jina lake yaani 'Roberto'.
Hivyo jina la ufukwe likafa akawa
anaitwa Roberto, hata alipomzaa Shaaban alipohamia mjini Tanga katika
shamba la Mikonge Amboni, mzee Roberto aliendelea kutumia jina hilo na
mwanae Shaaban akawa akiitwa Shaaban Roberto, lakini alipoanza shule kwa
kuwa alisoma shule za Kiingereza walimu wake wakawa hawawezi kutamka
'Roberto' wakawa wanamwita 'Robert' mwanzoni Shaaban alikuwa akiandika
jina lake kama Shaaban Roberts, lakini alipokuwa mtu mzima akawa
akijiita Shaaban Robert.
Alitumia maisha yake katika
kuandika fasihi ya Kiswahili kuanzia mashairi, riwaya, tamthilia na kila fani
iliyohusu fasihi andishi. Wataalamu wa lugha ya Kiswahili wanasema tangu
kufariki kwake tarehe 20 june, 1962 hakujatokea
mtu yeyote aliekitendea haki Kiswahili kama
alivyofanya Shaaban Robert katika uhai wake.
Baada ya kumaliza darasa la
11 Shaaban aliajiriwa na Serikali ya kikoloni wakati huo ikiitwa Tanganyika
akiwa karani. Kuanzia mwaka 1926 mpaka 1944 alikuwa afisa forodha katika
bandari mbalimbali nchini hasa Pangani na Bagamoyo, kuanzia mwaka 1944 mpaka
1946 alihamia mjini Morogoro katika ofisi ya mbuga za wanyama. Na kuanzia mwaka
1946 mpaka 1952 alihamia Tanga katika ofisi ya kupima ramani alipostaafu
utumishi wa umma.
Kutokana na umahiri wake wa
kuandika chama cha TANU kilimtumia katika shughuli zake akiwa mhamasishaji kwa
kutumia kipaji cha ushairi. Mwalimu Nyerere alivutiwa sana na umahiri wa Shaaban Robert hata katika
upande wa ushairi uliotukuka.
Katika tuzo alizopata
kutokana na umahiri wake wa kuandika ni Margaret Wrong Memorial Prize for
Writing, kadhalika utawala wa kiingereza ulimpa heshima ya uraia nchini
Uingereza kwa tuzo ya Member of the British Empire (MBE).
Katika maandishi yake shaaban
Robert alilenga sana
utu, nafasi ya mwanamke katika jamii, ukombozi wa bara la Afrika, kukuza lugha
ya Kiswahili, na maendeleo. Mwalimu Nyerere alimpa tuzo ya fasihi iliyotukuka
kutokana na mchango wake katika jamii ya Tanganyika
na Tanzania
baadae, lakini tayari alikuwa ameshafariki.
Mpaka anafariki kwa maradhi
ya moyo na upungufu wa damu, Shaaban Robert alifanikiwa kuandika vitabu 24 kwa
lugha adhimu ya kiswahili, na mpaka sasa kazi zake zinazidi kukusanywa na taasisi ya uchunguzi na kukuza Kiswahili
(TUKI) ya chuo kikuu cha Dar es Salaam. Kipo kitabu cha 25 ambacho kilitolewa
miaka ya karibuni mabacho kina barua alizokuwa akiandikiana na jamaa zake.
Post a Comment