0


Na Bashiru Kauchumbe,Ruangwa.
Jumla ya kaya 64 katika kijiji cha Mtondo wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi hazina  mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa kwa upepo mkali ulioambatana na mvua.

Pia katika tukio hilo la kusikitisha jengo la zahanati katika kijiji hicho liliezuliwa kwa upepo huo mazingira yaliyosababisha kusimama kwa huduma za afya kwa wananchi kijijini hapo.

Akisimulia mkasa huo kwa waandishi wa habari, Diwani wa Kata ya Nambilanje Adala Chigope alisema  kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita majira ya saa 1:00 usiku .

Alisema upepo huo mkali ulioambatana na   mvua kubwa iliyonyesha kijijini hapo imeleta athari kubwa kutokana na baadhi ya miundombinu ikiwemo barabara kuharibika vibaya.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ruangwa Mariam Mtima aliyeambatana  na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na usalama na wa kamati ya maafa wilayani humo aliuagiza uongozi wa serikali ya kijiji kufanya tathimini ka kumpelekea taarifa kwa ajili ya utekelezaji.

Alisema tukio hilo ni la kusikitisha na kwamba yeye kama mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya alifikia kijijini hapo kwa lengo la kuangalia hali halisi ya maafa hayo pamoja na kuwafariji waathirika.

“Nawaagiza uongozi wa kijiji pamoja na kata… kufanya tathimini ili kupata takwimu halisi za waathirika pamoja na mali zao ili nasi tuweze kutoa taarifa Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya aliwaondoa hofu wananchi wote walioathirika na mvua hizo na kwamba serikali iko pamoja nao huku akitoa rai kwa wananchi walionusurika kwenye tukio hilo kuwasaidia wenzao.


Ofisa  Mtendaji wa Kata ya Nambilanje Abdala Tamba alisema  kwa sasa kaya zilizoathirika zinatunzwa na ndugu na jamaa wakati wanasubiri msaada kutoka serikalini.

Post a Comment

 
Top