Klabu ya Yanga leo imemtambulisha rasmi
mchezaji wao wa kimataifa kutoka Niger Issoufou Boubacar Garba baada ya
kukamilisha usajili wa mchezaji huyo ambaye amesaini mkataba wa miaka
miwili kuitumikia Yanga kuanzia sasa.
Garba amesajiliwa siku chache kabla ya
dirisha dogo kufungwa baada ya benchi la ufundi la Yanga kujiridhisha na
kiwango chake kufuatia majaribio ya muda mfupi aliyofanya kwenye kikosi
hicho chini ya kocha mkuu Hans van Pluijm.
Garba amesema kila kitu kinakwenda sawa na
amewaahidi mashabiki wa Yanga kwamba, atapambana kuhakikisha anafanya
vizuri na kuisaidia Yanga kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali.
“Najisikia furaha tangu nimefika Tanzania
kujiunga na Yanga, kila kitu kinakwenda sawa kuanzia kwa kocha, wacheaji
pamoja na mashabiki. Yanga ni timu kubwa najivunia kucheza hapa na
nawaomba mashabiki wasubiri kuona kutoka kwangu”, amesema Garba.
Amepewa jezi namba 14 ambayo kabla yake
ilikuwa inavaliwa na beki wa kulia Joseph Zutta aliyesajiliwa kutoka
Ghana lakini mkataba wake na klabu hiyo ulivunjwa kwa kile kilichodaiwa
ni kushindwa kuonesha kiwango kilichotarajiwa na benchi la ufundi.
Mchezaji mwingine ambaye amesajiliwa na
Yanga katika kipindi cha dirisha dogo la usajili ni Paul Nonga ambaye
hakuwepo wakati wa utambulisho kutokana na kurejea kwenye klabu yake ya
amani ya Mwadui FC ya Shinyanga kwa ajili ya kuagana na timu hiyo na
kufanya taratibu za kuhamia jijini Dar es Salaam.
Post a Comment