SERIKALI
inachunguza ufisadi wa Dola za Marekani milioni sita, ambazo Benki ya
Stanbic Tanzania pamoja na Kampuni ya Egma ya nchini, iliongeza katika
malipo ya ada ya mkopo, ambao Serikali iliomba kwa Benki ya Standard ya
Uingereza mwaka 2013.
Imesema
inafanya uchunguzi wa ndani ili kubaini fedha hizo za kigeni
zilizoingizwa kwenye akaunti ya Egma, zimekwenda wapi na kama zilitumika
kuhonga, zimemhonga nani. Akizungumza na waandishi wa habari jana Ikulu
Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hatua
hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi
ya Uingereza (SFO) kushinda kesi katika Mahakama ya Southwark Crown ya
Uingereza dhidi ya Stanbic Tanzania inayomilikiwa na Standard Group.
“Sasa
baada ya Taasisi ya SFO kushinda kesi, Tanzania tunarudi kufanya
uchunguzi wa ndani kubaini hizo fedha dola milioni sita zilizoingizwa
kwenye akaunti ya kampuni ya Egma na kutolewa zote muda mfupi zimekwenda
wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu, ni nani,” alifafanua Balozi
Sefue.
Balozi
Sefue aliwataja wamiliki wa Egma kuwa ni aliyekuwa Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la
Mitaji Tanzania, Fratern Mboya na Mkurugenzi Gasper Njuu.
Alitoa
mwito kwa wamiliki hao, kutoa ushirikiano wakati wa uchunguzi wa sakata
hilo na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika, iwapo kutabainika
makosa ya rushwa au mengine, sheria itachukua mkondo wake.
“Ombi
letu na ombi la Rais John Magufuli watu hawa wanatakiwa kutoa
ushirikiano na pengine ameongezeka mmiliki kwenye kampuni hiyo,
wahakikishe wanatoa ushirikiano,” alisisitiza Balozi Sefue. Akizungumzia
sakata hilo, Balozi Sefue alisema sio jambo geni kama ambavyo baadhi ya
vyombo vya habari nchini vimeripoti jana, na kwamba tangu mwaka 2013,
Tanzania inalifahamu na ndiyo iliyolipeleka SFO kuchunguzwa.
Akifafanua,
alisema katika mwaka 2012/13, serikali ilifanya utaratibu wa kawaida
unaofanywa na nchi mbalimbali duniani wa kukopa kwenye taasisi za benki
ambapo Benki ya Standard ilikubali kuikopesha.
Alisema
katika mkopo huo, serikali ilihitaji Dola za Marekani milioni 600 kwa
ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo kwa kawaida
benki husika huingia mkataba na benki nyingine inayopewa jukumu la kutoa
mkopo huo.
Alisema
katika mchakato huo, Benki ya Standard kupitia kampuni tanzu iliipa
Benki ya Stanbic Tanzania kazi hiyo ambapo fedha hizo zilipatikana na
kwamba katika mchakato wa mkopo huo, ada ya mkopo serikali ilitozwa
asilimia 2.4 ya mkopo.
Aliyataja
masharti mengine kwamba yalikuwa ni kulipa mkopo riba kwa miaka saba,
na kwamba deni hilo litalipwa kwa miaka saba, ambapo linapaswa
kumalizika mwaka 2019. Balozi Sefue alifafanua kwamba baada ya mkopo
kutolewa nusu ya kwanza, Mtendaji Mkuu wa benki hiyo wakati huo, Bashir
Awale alikuwa na matatizo na watumishi, na Benki Kuu (BoT) iliingilia
kati na kufanya uchunguzi.
Katika
uchunguzi huo, kulibainika kasoro nyingi zikiwemo ulipaji wa fedha
kwenye kampuni bila maelezo ikiwemo Kampuni ya Egma ambayo ilibainika
kulipwa Dola za Marekani milioni sita.
Alisema
fedha hizo zilionekana zimeingizwa kwenye Egma na kutolewa zote bila
kutozwa kodi, ambapo katika taarifa yao ya ukaguzi, BoT ililionesha hilo
na mambo mengine yaliyobaini na kumkabidhi Mwenyekiti wa Benki ya
Stanbic Tanzania.
Hata
hivyo, baada ya taarifa hiyo kupokewa, mwenyekiti wa benki hiyo
aliitisha mkutano wa Bodi ya benki na waliipitia taarifa hiyo ya BoT na
taarifa kupeleka Kitengo ya Uchunguzi cha Kimataifa cha Intelijensia.
Alisema
katika uchunguzi huo, ndipo ilibainika kwamba nchi ilitozwa ada zaidi,
ambapo ada ya mkopo halali ilikuwa Dola za Marekani milioni 1.4, lakini
Stanbic walichukua Dola za Marekani milioni 2.4.
Alisema
fedha hizo zilizoamriwa na Mahakama nchini Uingereza kwamba Benki ya
Standard iilipe Tanzania ni zile ambazo hazikupaswa kuchukuliwa, ambazo
ni dola milioni sita na dola milioni moja ni faida.

Post a Comment