……………………………………………………………………………………………
WAZIRI
MKUU Kasim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu
kutoka nchi za China, Sudan Kaskazini na Korea Kusini.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti na mabalozi hao leo mchana (Jumanne, Desemba mosi,
2015), ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu
aliwashukuru mabalozi hao kwa pongezi walizokuja kumpatia na kuahidi
ushirikiano zaidi pamoja na nchi hizo.
Kwa
upande wake, balozi wa China, Dk. Lu Youqing alisema Serikali
itaendelea kuisaidia Tanzania kwenye sekta za uendelezaji viwanda,
miundombinu, maji, afya na elimu ikiwa ni ishara kuendeleza mahusiano
ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu baina ya China na Tanzania.
Alisema
Tanzania imeteuliwa kuwa miongoni mwa nchi tatu ambazo zitasaidiwa na
China kuendeleza viwanda na kwamba makubaliano ya mpango huo yatafikiwa
kwenye mkutano wa uwekezaji baina ya China na nchi za Afrika (FOCAC – 6)
unaotarajiwa kuanza Desemba 4, mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika
Kusini. Nchi nyingine mbili zitakazonufaika na mpango huo ni Kenya na
Ethiopia.
Naye
Balozi wa Sudan Kaskazini. Dk. Yassir Mohamed Ali alisema nchi yake
inao madaktari wengi na kwamba kumekuwa na majadiliano ya kuona ni jinsi
gani wanaweza kuja kuongeza nguvu kwenye sekta ya afya. “Tuna madaktari
wasiopungua 4,000 ambao wanahitimu kila mwaka na tungependa
kushirikiana na Tanzania katika eneo hili,” alisema.
Naye
Balozi wa Korea Kusini, Bw. Chung Il ambaye pia alitumia fursa hiyo
kuja kuagana na Waziri Mkuu Majaliwa, alisema anatumaini kuona ubalozi
wa Tanzania ukifunguliwa nchini mwao katika muda siyo mrefu.
Post a Comment