SIKU
moja baada ya Rais John Magufuli kuamuru fedha zilizotengwa kwa ajili
ya sherehe za Uhuru zikajenge barabara ya Bagamoyo kipande cha kilometa
4.3 cha Mwenge – Morocco, jijini Dar es Salaam, ujenzi huo umeanza jana.
Gazeti
hili lilishuhudia tingatinga mbili mali ya kampuni ya ukandarasi ya
Estim katika eneo la Mwenge, yakisafisha eneo la barabara hiyo, ikiwa ni
maandalizi ya upanuzi, kama maagizo ya Rais yalivyosema.
Dk
Magufuli juzi aliamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharamia sherehe za
Sikukuu ya Uhuru ambazo zingefanyika Desemba 9, mwaka huu, kutumika
kufanya upanuzi wa barabara hiyo ya Mwenge hadi Morocco kwa kuongeza
njia mbili za barabara za lami.
Aidha,
tayari fedha hizo Sh bilioni nne zimepelekwa kwa Wakala wa Barabara
(TANROADS) kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, ambalo limeanza
kutekelezwa mara moja kupitia mkandarasi huyo, Estim wa jijini Dar es
Salaam.
Dk
Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale
walipokutana Ikulu Dar es Salaam juzi, kuwa ujenzi wa barabara hiyo
uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika
barabara hiyo.
Mmoja
wa wasimamizi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya Estim ambaye hakutaka
kutaja jina lake, alipohojiwa na gazeti hili kuhusu kuanza kwa ujenzi
huo na utachukua muda gani, alisema taarifa zote zipo Tanroads.
Hata
hivyo, jitihada za kumpata Mfugale hazikuzaa matunda baada ya kutafutwa
mara kadhaa kwa simu na kuambiwa kuwa yupo kikaoni na wasaidizi wake
walisema yeye ndiye mwenye taarifa kamili.
Post a Comment