Dk Ackson alisema hayo hivi karibuni na kuongeza kuwa: “Mheshimiwa spika hayupo amesafiri nje ya nchi, atakaporejea kazi hiyo itafanyika.”
Hata hivyo, Dk Ackson hakutaja idadi ya kamati zitakazoundwa katika bunge hili la 11.
Alisema muundo wa kamati za bunge unategemea mahitaji ya wakati husika ndani ya Serikali pamoja na idadi ya wabunge.
Bunge lililomaliza muda wake Juni mwaka huu, lilikuwa na kamati 18 zilizojumuisha kamati za kudumu za bunge.
Kamati hizo ni za Uongozi, Kanuni za Bunge, Haki kinga na Madaraka ya Bunge, Ukimwi, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bajeti na Katiba, Sheria na Utawala.
Nyingine ni Uchumi, Viwanda na Biashara, Ulinzi na Usalama, Huduma za Jamii, Maendeleo, Miundombinu na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Bunge hilo pia lilikuwa na kamati za Hesabu za Serikali, Hesabu za Serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Nishati na Madini na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Alisema baadhi ya wabunge waliokuwa wameomba kuwapo kwenye kamati, wameteuliwa kuwa mawaziri na naibu mawaziri, hivyo kupoteza sifa.
Alisema nafasi zao zinapaswa kuangaliwa kwa kujazwa upya na wengine kulingana na mgawanyo utakavyokuwa.
Alisema kuwa ofisi yake inafanya utaratibu wa kujaza maeneo yatakayoonekana yanafaa kulingana na mahitaji.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tumaini Makene alisema viongozi wa Ukawa wako mbioni kuunda baraza kivuli litakalokuwa na nguvu ya kuwaonyesha Watanzania walichotakiwa kukifanya kama wangepewa ridhaa kwa Taifa hili.

Post a Comment