Na Shaffih Dauda, Osaka, Japan
Kesho mashindano ya FIFA Club World Cup yanaendelea tena kwa michezo miwili, mchezo wa kwanza utakuwa wa kutafuta mshindi wa tano na sita na utaikutanisha TP Mazembe dhidi ya Club America ya Mexico.
Timu ya Auckland City baada ya kufungwa na Sanfrecce Hiroshima kwenye mchezo wa kwanza wenyewe moja kwa moja wanashika nafasi ya saba na kutokana na kushika nafasi hiyo wanajinyakulia kitita cha dola laki tatu za kimarekani.
Licha ya kwamba timu zitakazomaliza nafasi ya tano na sita hazina nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo, lakini mzigo wa pesa unaowaniwa na vilabu hivyo ndiyo unaufanya mchezo huo kuwa na upinzani. Mshindi wa mechi kati ya TP Mazembe dhidi ya Club America ataondoka na dola milioni moja na nusu za kimarekani wakati atakaepoteza mchezo huo atachukua dola milioni moja za kimarekani.
Mchezo kati ya TP Mazembe dhidi ya Club America utaanza saa 4:30 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, baada ya mchezo huo mchezo utakaofuata ni kati ya River Plate kutoka Argentina dhidi ya Sanfrecce Hiroshima ya Japan mchezo huo ukisukumwa saa 7:30 kwa saa za Afrika Mashariki.
Timu ya River Plate itakuwa ikijaribu kufuta uteja kwenye michuano hiyo ambao umekuwa ukizikabili timu zinazotoka Argentina. Kwahiyo ni nafasi kwa River Plate kuandika historia kwenye michuano hiyo kwa kuwa timu ya kwanza kutoka Argentina kutwaa ubingwa kwasababu timu nyingine zimeshafika fainali na kupoteza michezo yao.
Sanfrecce Hiroshima wameonesha mchezo mzuri katika mechi zote mbili mpaka sasa wakiwa wameshafunga magoli matano huku wakiwa hawajaruhusu wavu wao kutikiswa lakini aina yao ya uchezaji ikiwa imewafanya wafike hatua hiyo ya nusu fainali.
Nimeongea na Thomas Ulimwengu nikitaka kujua hali ilivyo kwenye kambi ya TP Mazembe baada ya kupoteza mchezon wao wa robo fainali.
Shaffihdauda.co.tz: Baada kupoteza mchezo wa kwanza, jana jioni mmefanya mazoezi na leo mmefanya warm-up. Ni kitu gani kimejadiliwa na kocha pamoja na benchi la ufundi kwa ujumla kuhusu mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza.
Ulimwengu: Kocha bado hajazungumza na wachezaji kuhusiana na mechi ya kesho lakini nahisi kesho katika kikao ataongelea hayo mambo na tutajua nani anacheza nani hachezi, mapungufu yapi yalitokea kwenye mchezo wa awali lakini kikubwa tulionekana hatupo kitimu sana kwenye mchi iliyopita.
Shaffihdauda.co.tz: Moja kati ya matatizo ambayo yamezungumzwa sana kutokana na kichapo ambacho mlikipata kwenye mchezo wa robo fainali ni pamoja na wachezaji kucheza bila ushirikiano na kulikuwa na ubinafsi miongoni mwenu. Walio wengi wanadhani kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi kitakachocheza mechi dhidi ya Club America. Kwa mtazamo wako unadhani kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi kitachoanza ukilinganisha na kile kilichoanza kwenye mchezo wa robo fainali?
Ulimwegu: Nadhani yatakuwepo kwasababu naamini kocha atakuwa ameona kulikuwa na mapungufu sehemu gani, kwahiyo anaweza akajaribu kuangalia wachezaji wengine au akabadilisha mfumo wa mchezo. Lakini nahisi mabadiliko yanaweza kuwepo.
Shaffihdauda.co.tz: Hali ya hewa inaweza ikawa imewasababishia ugumu wa ushiriki wenu kwenye mashindano haya?
Ulimwengu: Haijatuathiri chochote kwasababu tumekuja mapema japo kama tungekaa kuanzia wiki moja na zadi tungezoea zaidi lakini inazoeleka tu kama sasahivi hali ya hewa tumeanza kuizoea kabisa, mimi naona hali ya hewa haikutuathiri kwa chochote.
Post a Comment