0


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kampus ya Mwl. Julius K. Nyerere kimeanzisha Shule ya Sayansi za Afya (School Of Health Sciences) ili kukabiliana na uhaba wa wataalam wa afya.

Akizungumza na wanahabari leo Kaimu Mkurugenzi wa Shule ya Afya, profesa Lawrence Mseru amesema Udsm ilianzishwa kutoa elimu katika fani zote ili kupiga vita dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi lakini kutokana na mabadiliko fani nyingi zilijitegemea na kuwa chuo ikiwemo Chuo Kikuu cha Sayansi ya afya Muhimbili (Muhas) hiyo kukifanya chuo kupoteza nguzo yake moja ya kutoa elimu ya juu kwa madaktari na wataalamu wengine wa afya.

Ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha sekta ya afya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari na wataalamu wengine wa afya kwa asilimia 60 ambao unafanya uwiano wa daktari kuhudumia wagonjwa wengi zaidi kuliko 10,000 kama inavyoshauriwa na shirika la afya duniani (WHO).

Profesa Mseru amesema kuwa kutokana na sababu hizo zimekifanya Udsm kuanzisha Shule ya Sayansi za Afya ya Chuo hicho ikianzia na kozi ya udaktari ambayo inaanza mwaka huu wa mafunzo 2015/2016 na tayari wanafunzi 150 walioidhiniwa na tume ya taifa ya vyuo vikuu wamesajiliwa.

“Kuna wanafunzi wengi wanaomaliza na kupata nafasi ya kujiunga na masomo ya afya lakini chuo kimoja hakitoshi kuwapeleka wote kwa hiyo unakuta wanaokuwa wanamaliza hawawezi kukidhi mahitaji ya madaktari wanao hitajika,” amesema profesa Mseru

Wakati huohuo Udsm imeanzisha shule mpya ya Sayansi na Teknolojia ya Kilimo na Uvuvi ambayo ina idara tano za shahada ya kwanza ambazo ni sayansi ya teknolojia ya maji na uvuvi, uhandisi kilimo na matumizi ya zana za kilimo, sayansi na teknolojia ya chakula, uchumi na biashara ya kilimo pamoja na teknolojia  ya ufugaji nyuki.

Profesa Masudi Muruke amesema wamefanya utafiti wa mahitaji ya soko la ajira  kwa fani wanazotoa bado kuna pengo kubwa la wataamu  hao pia programu zinalenga kuwapa wahitimu ujuzi wa kujiajiri na kuwaajiri wengine aliongeza kuwa watanzania wategemee  kupokea wataalamu wa kilimo waliopikwa kulingana na mahitaji ya kilimo.



Post a Comment

 
Top