MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaomba viongozi
wa dini kuiombea Zanzibar ili dosari zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu
zipatiwe mwafaka wa kiungwana.
Akizungumza katika ibada maalumu ya kumshukuru Mungu
kwa kudumisha amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi iliyofanyika kwenye
Ukumbi wa Diamond Jublee, Dar es Salaam jana, Samia alisema kwa hali ya kisiasa
iliyopo Zanzibar, ni dua za Watanzania za kumlilia na kumwangukia Mungu
zinazotakiwa ili kudumisha amani visiwani humo.
“Maombi yenu hayawezi kupotea bure. Kwa dua zenu
dosari ndogo zilizojitokeza huko Zanzibar zitapatiwa mwafaka wa kiungwana hivi
karibuni,” alisema Samia katika ibada hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Amani ya
Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kanisa la Agape.
Alisema kutokana na uchaguzi wa mwaka huu kukabiliwa
na changamoto kadhaa, kuna watu waliamini kuwa Tanzania isingetoka salama.
“Naamini bado Mungu anawapenda Watanzania jambo hilo limemalizika kwa salama na
amani,” alisema.
Alitoa mwito kwa Watanzania wote kulinda na kudumisha
amani na pia akasema jambo hilo lisifanyiwe mzaha na mtu yeyote, kwani amani
ikitoweka taifa litapukutika na kutoweka pia.
Alisisitiza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha
wanasimamia kikamilifu amani na hawatafanya mzaha na mtu yeyote yule ambaye kwa
maslahi yake au kikundi kidogo, atadiriki kuvuruga amani ya Watanzania walio
wengi.
Pia aliwakumbusha waumini wa dini zote nchini
kuendelea kupendana na kuvumiliana kiimani na kwamba tofauti zao za kiimani au
kuabudu haziondoi haki yao ya kuwa watoto wa baba mmoja ambaye ni Mungu na
kwamba nyumba yao ni moja, yaani Tanzania.
“Hakuna dini bora kuliko zingine. Dini zote ni sawa,
tofauti yake ni utaratibu na namna ya kuabudu. Pendaneni kwani dini zetu zote
zinatufundisha kuwapenda hata maadui wanaotuudhi,” alisema Samia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Alhad Musa Salum,
alisema kabla ya uchaguzi kamati hiyo ilihubiri amani na kuwaomba wananchi
wadumishe amani hivyo, jana walikuwa wanamshukuru Mungu kwa kusikiliza maombi
yao.
Shekhe Hemed Jalala akizungumza kwenye ibada hiyo
alisema Serikali ikiwa karibu zaidi na viongozi wa dini ana hakika nchi
itaendelea kubakia kisiwa cha amani na taifa halitambagua Muislamu au Mkristo.
Kiongozi wa Agape, Dk Venon Fernandes alisema
wamefanya ibada hiyo kwani sio vizuri kuendelea na biashara baada ya uchaguzi
bila kumshukuru Mungu kwa kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu.
Alisema kupitia kituo chake cha televisheni kuanzia
mwaka jana waliwaomba watu mbalimbali wajitokeze kuliombea taifa hili linapoelekea
kwenye uchaguzi mkuu na Mungu amesikia maombi yao. “Inabidi tumshukuru Mungu
kwa amani hii, hatuwezi kuendelea na biashara zetu bila kutoa shukrani,”
alisema Dk Fernandes.
Post a Comment