Edward Lowassa.
Edward Lowassa, amehoji maswali matatu kwa Rais Dk. John
Magufuli.Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam
jana, Lowassa amemtaka Rais Magufuli baada ya kusema hakuna mtoto
atakayelipa ada kuanzia Januari, mwakani, atamke mustakabali wa
wanafunzi walioko shuleni kama wataguswa na hatua hiyo au la.
Lowassa amesema kwa upande wake ahadi ya elimu bure aliyokuwa
akiinadi wakati wa kampeni, ilikuwa ni kuanzia shule ya awali hadi chuo
kikuu na kwamba hata wale walioko mashuleni, wangeguswa na hatua hiyo.
“Niliahidi watoto wote walioko na watakaoanza shule kuanzia
kindergarten (shule ya awali) hadi chuo kikuu, serikali yetu
ingegharimia. Na nilitangaza kufuta michango yote shuleni ili
kumpunguzia mzigo mwananchi,” alisisitiza Lowassa ambaye amekataa
kuyatambua matokeo ya ushindi wa Dk. Magufuli akidai kuwa yeye ndiye
aliyeshinda kwa asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa.
Kuhusu suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Lowassa
amesema yeye alishaweka wazi kuwa elimu ingekuwa bure hadi chuo kikuu.
“Vijana hawa wanahangaika na mikopo na nasikia ni asilimia 17 tu
kati ya wanafunzi 70,000 ndiyo waliopata mikopo. Sera ya Chadema na
Ukawa kwa ujumla, ni kufuta kabisa shida hizi kwa serikali kufadhili
elimu yao,” alifafanua Lowassa katika taarifa yake hiyo. Kwa msingi huo,
Ukawa kupitia kwa aliyekuwa mgombea wao wa urais, Lowassa, umewataka
wananchi kutofautisha ahadi ya elimu bure iliyotolewa na Rais Magufuli
na ile iliyotolewa na Ukawa.
Lowassa alisema Magufuli ametoa maelekezo kwa watendaji wa serikali
kuweka mikakati ya kutekeleza ahadi yake kuanzia Januari, mwakani
kwamba hakuna mtoto atakayelipa ada.
Hata hivyo, amesema hajaeleza waziwazi hatma ya wanafunzi walioko mashuleni kama wataguswa na hatua hiyo au la.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment