0


 Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman ametuma wapelelezi mkoani Kilimanjaro, kuchunguza mauaji ya kinyama ya James Massawe aliyeuawa mwaka 2009.

Uamuzi huo wa DCI umekuja siku moja baada ya gazeti hili kuchapisha taarifa za ndugu wawili wa marehemu; Beda Massawe na Peter Massawe, kumwandikia barua Rais John Magufuli wakimwomba aingilie kati suala hilo.

Ndugu hao walimwandikia barua Rais Magufuli baada ya matajiri wanne wa jijini Mwanza wanaodaiwa kufanya mauaji hayo na baadaye kutorokea Uarabuni, kurejea nchini na kuendelea na biashara zao.

Marehemu James, aliuawa hadharani na matajiri hao mwaka 2009 huku jalada la uchunguzi lililokuwa na nyaraka muhimu yakiwamo maelezo ya mashuhuda likitoweka mikononi mwa polisi.

Mbali na kuibwa kwa jalada hilo lililokuwa pia na taarifa ya uchunguzi wa kifo cha marehemu, majalada mengine manne ambayo yalikuwa ni nakala ya jalada halisi nayo yaliibwa ofisi tatu tofauti za umma.

Yaliibwa katika ofisi ya mkuu wa upelelezi (RCO) Mkoa wa Kilimanjaro, ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.

Hata hivyo, jana DCI aliliambia gazeti hili kuwa tayari ametuma timu ya wapelelezi kutoka ofisi yake kwenda kukusanya ushahidi wa tukio hilo na kuwaomba walioshuhudia watoe ushirikiano.

“Ni azma ya ofisi hii kuona jambo hili linafikia mwisho. Tunahitaji kuijenga kesi, maana kitakachotusaidia ni uimara wa ushahidi wetu,” alisema DCI Athman na kuongeza;

“Tunahitaji ushirikiano baina ya mashahidi wetu wa mashtaka na timu niliyoipa kazi hii kutoka hapa makao makuu ya upelelezi ambayo tayari inahangaika kuwapata mashahidi hivi sasa”.

Katika barua yao ya Novemba 13 waliyomwandikia Rais Magufuli, ndugu hao wa marehemu walisema, “Tumeshalalamika kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini, mwanasheria mkuu wa serikali, mkuu wa jeshi la polisi na kwa DCI bila kupata msaada wowote.

“Tunakuandikia barua hii, tukiwa wanyonge na tuliokata tamaa kutokana na namna watuhumiwa wanne tuliowashuhudia wakimuua kinyama ndugu yetu wakiwa mitaani.”

Katika barua yao hiyo, ndugu walidai baada ya kufunguliwa kwa kesi ya mauaji namba PI 9/2009, watuhumiwa hao muhimu walitoroka hadi kesi ilipofutwa mwaka 2012 baada ya kukosa nguvu.

“Leo hii baada ya kupita ya takribani miaka sita, watuhumiwa hao wamerejea jijini Mwanza na wanaendelea na shughuli zao za kibiashara kama kawaida, utadhani hawakuwa wanatafutwa,” inasema sehemu ya barua hiyo

Katika hatua nyingine, washtakiwa saba katika kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya, wamefuta mpango wao wa kwenda Mahakama ya Rufaa kupinga maamuzi madogo yaliyotolewa na Jaji Salma Maghimbi.

Jaji Mkuu, Othman Chande amekubali ombi la kuondoa notisi yao ya kukata rufaa, kupinga kupokelewa kwa maelezo ya mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu kama kielelezo cha kesi hiyo.

Katika maelezo hayo ya onyo yaliyoandikwa na Ofisa wa Polisi Inspekta Msaidizi, Herman Ngurukizi, mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kwa ufasaha mipango ya mauaji ya Msuya.

Ni kutokana na maamuzi hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Bernard Mpepo, aliliambia gazeti hili jana kuwa kesi hiyo sasa itaendelea kusikilizwa mfululizo kwa wiki tatu kuanzia Januari 18, 2016.

Jaji Maghimbi alisimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo Oktoba 19 baada ya mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu kuwasilisha notisi hiyo.

Walikuwa wanapinga kupokelewa kama kielelezo kwa ripoti ya uchunguzi wa daktari kuhusu kifo cha Msuya na pia kutupwa kwa pingamizi lao kuhusu muda aliokamatwa mshitakiwa.

Post a Comment

 
Top