Miili ya wanajeshi 10 wa Uganda,
waliouawa na wapiganaji wa al-
Shabaab, nchini Somalia
imesafirishwa nyumbani.
Msemaji wa jeshi, Kanali Paddy
Ankunda, amesema shambulio hilo
"limebadili mambo" na al-Shabaab
wanafaa kutarajia "jibu lifaalo".
Wanajeshi 12 wa Uganda
waliuawa kwenye shambulio hilo
la Jumanne, kwenye kambi ya
wanajeshi wa Muungano wa Afrika
(AU) Kusini mwa Somalia.
Al-Shabaab walisema waliua
wanajeshi 70 wa AU.
Wanajeshi wa Uganda wamo
kwenye kikosi cha wanajeshi
22,000 cha AU, kinachokabiliana
na wapiganaji hao nchini Somalia.
Kwenye tamko la kwanza kabisa
kutoka kwa jeshi la Uganda
kuhusu shambulio hilo, Kanali
Ankunda alisema kupitia mtandao
wa kijamii wa Twitter:
"Hatutalegeza juhudi zetu za
kusaidia kurejesha amani Somalia
licha ya shambulio hilo." Hakutoa
maelezo kuhusu miili ya wanajeshi
hao wengine wawili waliouawa.
Ripoti nyingine zinakadiria
wanajeshi waliouawa kwenye
uvamizi huo katika kambi ya
Janale, kilomita 90 Kusini
Magharibi mwa mji mkuu
Mogadishu, ni kati ya 20 na 50.
Wakazi wanasema shambulio hilo
lilianza kwa shambulio la kujitoa
mhanga lililotekelezwa kwa
kulipua gari lililotegwa bomu
kwenye lango la kambi hiyo, na
kisha kukawa na ufyatulianaji wa
risasi uliodumu zaidi ya saa moja.
Licha ya kupoteza ngome nyingi
kusini na kati mwa Somalia, al-
Shabaab wameendelea
kushambulia vikosi vya serikali na
Muungano wa Afrika pande
mbalimbali nchini humo.
Wapiganaji hao pia hutekeleza
mashambulio ya mara kwa mara
ya kujitoa mhanga Mogadishu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment