0
                                      
Historia ya Mgonjwa
Mnamo tarehe 9 Agosti 2015, mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 kutoka katika kambi
ya  wakimbizi ya Nyarugusu  alipokelewa  katika  hospitali  ya  Mkoa  wa  Kigoma  Maweni
akiwa na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili hasusan kwenye fizi,
macho na masikio. Vile vile alikuwa na dalili za kuchoka na mwili kuwasha. Mgonjwa
huyu  hakuwa  na  homa. Alipata  matibabu  katika  hospital  hiyo  na  kwa  bahati  mbaya
mnamo tarehe  10  Agosti,  2015  mgonjwa  huyu  alifariki dunia. Mgonjwa  huyu alikuwa
hana  historia  ya kusafiri  kutoka  nje  ya  mkoa  wa  Kigoma wala  kutembelewa  na  mtu
aliyesafiri kutoka nchi za Afrika Magharibi zenye ugonjwa wa Ebola.
Mgonjwa huyu alikuwa ni mkimbizi wa kutoka nchi ya Burundi ambaye ameishi katika
kambi  ya  Nyarugusu  kwa  miaka  mitatu.  Mgonjwa huyu  alikuwa  mmojawapo  wa
wakimbizi  waliokuwa  wasafirishwe  katika  mpango wa  kawaida  chini  ya  Shirika  la
Kimataifa linalohudumia wakimbizi kwenda Marekani. Safari hiyo ilikuwa ianze tarehe 9
Agosti 2015.
Hatua zilizochukuliwa
1.  Mgonjwa  huyu  alipatiwa  matibabu  katika  hospitali ya  Maweni  Kigoma  mpaka
mauti ulipomkuta.
2.  Uongozi wa Afya Kigoma unafuatilia ndugu wa karibu wa mgonjwa huyu, pamoja
na  wahudumu  wa  Afya  waliomuhudumia  mgonjwa  huyu  kuona  kama
wataonyesha  dalili  zinazofanana  na  ugonjwa  aliokuwa  nao  mgonjwa  huyu.
Ufuatiliaji huo umeanza tarehe 9 Agosti 2015. Mpaka leo hakuna mtu mwingine,
aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu.
3.  Sampuli  ya  mgonjwa  huyu  imechukuliwa  na  kupelekwa  kwenye  maabara  ya
Taifa ya  Afya  ya  Jamii,  ya  Wizara ya  Afya  na  Ustawi  wa  Jamii  iliyopo  Dar  es
Salaam kwa uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha ugonjwa huu.
4.  Mazishi ya marehemu huyo yamefanyika chini ya uangalizi wa Afya mkoa, kwa
kuzingatia Utaratibu wa Kanuni za Kimataifa za kuzuia maambukizi.
Hitimisho
Wizara  ya  Afya  na  Ustawi  wa  Jamii  inapenda  kuwahakikishia  wananchi  kuwa  mpaka
sasa, hakuna uthibitisho wowote kuwa mgonjwa huyu amekufa na ugonjwa wa Ebola.
Aidha  kwa  kuwa  ugonjwa  bado  unaendelea  nchi  za  Afrika  Magharibi, Wizara inazidi
kusisitiza  wananchi  kuchukua  tahadhari  za  kujikinga  na  ugonjwa wa  Ebola  na
magonjwa mengine ya kuambukiza. Ikiwa ni pamoja na
o  Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na
majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa
wa Ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
o  Kuepuka kushughulikia  maiti  ya  mtu  aliyekufa  akiwa  na  dalili  za  ugonjwa  wa
Ebola;  badala  yake  watoe  taarifa  kwa  uongozi  wa  kituo  cha kutoa huduma  za
Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa kifo kitatokea.
o  Wananchi  waepuke  mila  na  desturi zinazoweza  kuchelewesha  kupata  huduma
muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
o  Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika
ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
o  Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na
dalili za ugonjwa huu.
o  Kunawa  mikono  mara  kwa  mara  ili  kuepuka  kusambaza  ugonjwa  ikiwa  mtu
atakuwa ameshika mgonjwa au mazingira yenye maambukizi.
o  Kutumia kemikali za kuua vijidudu kutakasa mikono.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itatoa taarifa pindi majibu ya maabara
yatakapopatikana.
BOFYA HAPA KUIPATA TAARIFAA HII

Post a Comment

 
Top