Sukari ya ndani ikipewa uzito, ni dhahiri mashamba ya miwa kama hili
yataendelezwa na hivyo kuchangia uchumi wa Taifa. Picha ya Maktaba.
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16, iliyosomwa
bungeni na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya inaainisha mpango wa makusudi wa
Serikali wa kuizuia sukari kutoka nje ya nchi kuingia katika soko la
ndani kirahisi.
Katika mpango huo, Mkuya
anasema kuwa ushuru kwa sukari kuingia nchini utaongezeka kwa zaidi ya
mara mbili ya kiwango kilichokuwa kinatozwa mwaka uliopita.
Mtu
anaweza kujiuliza, nini maana ya mpango huo? Je una tija kwa wananchi
na taifa kwa jumla? Ili kuweza kufahamu vyema hali hii ni vyema ukapata
majibu namna mpango huu unavyoweza kutoa manufaa kwa taifa, viwanda na
wakulima wa miwa. Kabla ya kujua hayo ni vyema ikafahamika hali halisi
ya uzalishaji pamoja na matumizi.
Uzalishaji sukari
Takwimu
za Wizara ya Kilimo na Chakula, zinaonyesha kuwa mahitaji ya sukari
nchini, kwa matumizi ya nyumbani ni tani 590,000 kwa mwaka wakati
uzalishaji ni wastani wa tani 300,000. Uzalishaji huu ni sawa na nusu ya
mahitaji.
Hii pekee kiuchumi inaonyesha kuwa zipo fursa za uwekezaji, kuongeza ajira na kuimarisha sekta ya viwanda na kilimo nchini.
Ripoti
ya hivi karibuni iliyotolewa na Kampuni ya Nishati na Kilimo cha Miwa
ya Agro EcoEnergy (T) Ltd inaeleza kwamba Serikali ikiweka vizuri
mipango yake katika sekta ya sukari, inaweza kupiga hatua kubwa ya
maendeleo na kupunguza umaskini.
Kwanza inaelekeza kuwa
Tanzania ina ardhi ya kutosha inayoweza kuzalisha miwa kwa wingi. Hii
ni fursa inayoweza kuwanufaisha wakulima wengi kwa sababu viwanda
vitanunua miwa kwa wingi na vitashirikiana na wazalishaji kuboresha zao
hilo.
Jambo jingine ni kwamba sekta ya Sukari nchini
inajiuza yenyewe kwa sababu soko kubwa lipo, hivyo wenye mitaji mikubwa
hawatakuwa na wasiwasi kwamba wanaweza kupata hasara.
Kwa
sababu hiyo, Agro EcoEnergy wanaamini kuwa Serikali ikijenga mazingira
mazuri, viwanda vya sukari nchini vitakua na kuongezeka na vitaongeza
ajira ya maelfu ya watu.
Jambo jingine la faraja katika
mpango huo ni kwamba mabaki ya miwa yatakayozalishwa na viwanda
yatatumika kuzalisha umeme kwa kuwa ni chanzo kizuri cha nishati hiyo.
Kwa
kuwa Serikali tayari imezuia sukari ya nje kuingia nchini kiholela ina
maana kwamba sasa mazingira mazuri kwa mpango huo wa Agro EcoEnergy,
unaweza kutekelezeka.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Sukari
Kagera, Ashwiin Rawa anasema kuwa endapo wananchi wataiona fursa ya
kujikwamua kiuchumi iliyopo kwenye sekta hiyo, taifa linaweza kusonga
mbele na kujitosheleza na hata kuwa na ziada ya kuuza nje.
Rawa
anaeleza kuwa licha ya kiwanda hicho kilichopo chini ya mwekezaji,
Super Group of Companies kutilia mkazo kilimo cha umwagiliaji,
kinawategemea zaidi wakulima wadogo wanaokizunguka.
Kuyumba kwa bei ya Sukari
Meneja
wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Hamad Yahya anasema kuyumba kwa bei ya
sukari nchini kunatokana na wafanyabiashara wanaokwepa kodi na huuza
bidhaa kwa bei ya chini.
Kitendo hicho huwasababishia hasara wazalishaji wa ndani, inayotokana na kupata kidogo kuliko gharama za uzalishaji.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana alipotembelea
Mtibwa wakati akiwa kwenye ziara yake ya kuizungukia mikoa ya Kanda ya
Ziwa, anasema katika moja ya mambo ambayo chama kinayahimiza sasa kwa
nguvu zote ni lazima uwekezaji uwe ni kwa ajili ya kuwanufaisha
wananchi.
“Nimesikia kilio chenu juu ya magendo na
naahidi kuishauri serikali ya chama changu kuchukua hatua juu ya jambo
hilo ili kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na serikali yenyewe,”
alisema Kinana.
Mipango ya kinana imekuja kuonekana
wazi kwenye bajeti ya mwaka huu, ambayo inaweka mikakati ya kuzuia
sukari inayotoka nje, hasa kwa magendo, ili kuimarisha viwanda na
kuongeza ajira viwandani na kwa sekta ya kilimo cha miwa.
Kudhibiti sukari ya magendo
Mkutano
uliofanyika Morogoro, ukiwakutanisha wadau na Serikali na wadau wa zao
la sukari, ilipendekezwa Serikali kudhibiti sukari ya magendo.
Pamoja
na hilo, iliafikiwa kuwa Serikali isimamie mfumo mzima wa usambazaji wa
bidhaa hiyo nchini ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wafanyabishara wenye
tabia ya kuhodhi soko lake kwa lengo la kusababisha upungufu usio
halisi.
John Mzee, mkulima wa zao hilo kutoka Kilombero
mkoani Morogoro anasema kuwa familia yake imekuwa ikiendeshwa kwa
kutegemea kilimo cha miwa kwa muda mrefu.
Anafafanua
kuwa kuna wakati wakulima wadogo huzalisha kwa wingi kiasi cha kukosa
soko la uhakika hivyo akasema wakulima wengi watafaidika iwapo viwanda
vitaongezwa.
Anasema kuongezeka kwa viwanda vya sukari
kutahamasisha wengi kuingia katika kilimo hicho na kitawasaidia katika
kuongeza kipato na hata utajiri.
“Mimi na ndugu zangu
wote tumesoma kupitia kilimo hiki. Ninakifahamu vizuri kwani nimekuwa
nashirikiana na familia yangu kukiendesha.
“Kama soko
lingekuwa linaeleweka tungekuwa wakulima wakubwa sana. Viwanda
viongezwe, ushindani utatufaidisha, tutatajirika,” anasema John.
Serikali
sikivu ni ile inayosikiliza wananchi wanataka nini, jambo gani
litawafaidisha na kulitekeleza. Bila shaka kitendo cha Serikali
kusikiliza kilio na kukiingiza kwenye bajeti kwa mikakati ya utekelezaji
ni jambo zuri lenye manufaa kwa taifa.
Kilichobaki ni
kuendelea kusimamia utekelezaji kwa kuzuia sukari ya nje kuingia
kiholela kwenye soko la ndani. Ni matarajio ya Watanzania kuwa baada ya
miaka michache wawekezaji katika sekta ya sukari wataongezeka na ajira
za viwandani na kilimo, nazo zitakuwa nyingi na kuwafanya wananchi wengi
kuondokana na umaskini.MWANANCHI
Post a Comment